Nchi za Tanzania na Uturuki
leo zimetiliana saini mikataba tisa ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali za
kimaendeleo.
Akizungumza baada ya kutiliana
saini mikataba hiyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli
amesema, ujio wa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan umejumuisha
wafanyabiashara 150 na kwamba, mikataba iliyosainiwa itasaidia kukuza uchumi
pamoja na mahusiano baina ya mataifa hayo mawili.
Rais Magufuli ameitaja
baadhi ya mikataba iliyosainiwa kuwa ni ya sekta za afya, elimu, ulinzi, na
viwanda ambapo amesema, amemuomba Rais Erdogan kuikopesha Tanzania kiasi cha
fedha kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge yenye urefu wa
zaidi ya kilometa 400.
Rais Magufuli pia amesema
Rais huyo wa Uturuki amekubali kuongeza nafasi za wanafunzi wanaokwenda kusoma
nchini Uturuki kutoka idadi ya wanafunzi 48 iliyopo hivi sasa, na katika
masuala ya ulinzi, amesema Uturuki imekubali kutoa mafunzo ya ulinzi kwa
watanzania nchini Uturuki.
Hadi sasa kampuni 30 za
Uturuki zimefanya uwekezaji nchini Tanzania wenye thamani ya Dola za Kimarekani
milioni 305.08 na zinatarajiwa kutengeneza ajira 2,959 na hadi kufikia
Februari 2016 biashara kati ya nchi hizi mbili iliongezeka kutoka Dola za
Marekani milioni 66 sawa na shilingi bilioni 145.2 mwaka 2009 na kuwa
Dola za Kimarekani milioni 160 sawa na shilingi bilioni 352.
Post a Comment