0
Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili hapa nchini tarehe 22 na 23 Januari 2017 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
 
Mhe. Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan 

Rais Erdogan ambaye ataambatana na Mkewe, na kuongoza ujumbe wa watu 150 wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Maafisa kutoka Serikalini na Wafanyabiashara anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jioni  ya leo na atapokelewa na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Uturuki na Tanzania pamoja ‎na kupanua fursa za uwekezaji hususan katika maeneo ya biashara  na uwekezaji.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Erdogan  atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa  na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili na baadaye Marais hao watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali.

Siku hiyo ya tarehe 23 Januari, 2017, kutakuwa na Kongamano la Biashara kati ya Uturuki na Tanzania litakalowakutanisha Wafanyabiashara kutoka nchi hizi mbili. Kongamano hilolitahutubiwa na viongozi wa Tanzania na Uturuki.

Mhe. Rais Erdogan na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.


Post a Comment

 
Top