0
 surgical scissors
Madaktari nchini Vietnam wametoa mkasi wa kufanyia upasuaji kutoka kwenye tumbo la mwanamume mmoja baada ya kukaa na mkasi huo kwa miaka 18.
Wataalamu wa upasuaji walisafiri kwa ndege kutoka mji mkuu wa Hanoi kusaidia katika upasuaji huo uliofanyika katika mkoa wa Thai Nguyen kaskazini mwa nchi hiyo.
Mgonjwa huyo wa umri wa miaka 54 alifika hospitalini baada ya kuhusika kwenye ajali ya barabarani mwezi jana.
Lakini baada yake kupigwa picha ikagunduliwa kwamba alikuwa na kifaa cha chuma chenye ncha kali sehemu ya kushoto tumboni.
Alipimwa tena katika hospitali iliyo karibu katika mkoa jirani wa Bac Kan na ikabainika bila shaka kwamba alikuwa na mkasi wa urefu wa sentimita 15 (inchi 6) karibu na utumbo wake mkubwa, gazeti la Tuoi linasema.
Ma Van Nhat anasema huenda mkasi huo uliachwa mwilini mwake alipofanyiwa upasuaji katika hospitali kuu ya mkoa wa Bac Kan mwaka 1998 baada yake kuhusika katika ajali nyingine ya barabarani, kwa mujibu wa gazeti la Vietnam Express.
Hakuwa amepata tatizo lolote la kumfanya agundue alikuwa na kifaa hicho tumboni ila majuzi tu alipoanza kuhisi maumivu makali tumboni.
Alijaribu kunywa dawa za kutuliza maumivu lakini uchungu huo haukuisha.
Wataalamu waliomfanyia upasuaji kwa muda wa saa tatu walisema mkasi huo uliokuwa umeshika kutu baadhi ya sehemu zake ulikuwa umekwama na kushikana na baadhi ya viungo tumboni.
Wizara ya afya nchini humo imeagiza hospitali ya Bac Kan kutoa taarifa kuhusu nani huenda aliacha mkasi huo kwenye tumbo la Bw Ma kufikia mwisho wa wiki.
Mkurugenzi wa hospitali hiyo amesema atafanya kila awezalo kutimiza hilo.
Lakini madaktari wameambia Tuoi Tre kwamba ni nadra sana kwa hospitali kuhifadhi nyaraka kwa zaidi ya miaka 15.
Bw Ma, anatarajiwa kurejea nyumbani wiki ijayo baada ya kupata nafuu.

Post a Comment

 
Top