Siku moja baada ya Mkoa wa Mtwara kutangazwa kushika mkia katika
matokeo ya upimaji wa kitaifa wa wanafunzi wa kidato cha pili, Mkuu wa
Mkoa huo, Halima Dendego amesema hayajatokea kwa bahati mbaya.
Mkuu huyo alisema licha ya kutofurahishwa na matokeo hayo, alitarajia
hali ingekuwa hivyo kutokana na suala la elimu kutopewa kipaumbele
mkoani Mtwara.
Alisema tangu ateuliwe kuongoza mkoa huo, amegundua kuwa mambo mengi
hayaendi sawa katika elimu, hali iliyomlazimu kujiwekea mikakati ya
kujipanga upya.
“Nimekuja Mtwara nimegundua mambo hayako sawa, nikajaribu kutafuta
kiini, ndiyo nikabaini hakuna mwamko wa elimu, walimu siyo wabunifu.
"Wanashindwa kuangalia mazingira yaliyopo na kufundisha kulingana nayo. Utoro pia umekithiri,” alisema.
Aliitaja changamoto nyingine aliyoigundua kuwa ni udanganyifu kwenye
mitihani hasa ya kuhitimu elimu ya msingi ambayo watoto wengi hufaulu
kwenda sekondari.
“Hao watoto waliofanya mtihani wa kidato cha pili mwaka jana walifaulu
vizuri mtihani wa darasa la saba iweje leo washindwe, hapo ndipo
utagundua kuna mazingira ya udanganyifu.
“Watoto wengi wameingia sekondari kwa udanganyifu kwa hiyo matokeo haya
tuliyajua, jambo hili nimedhamiria kulikomesha lengo langu ni kuuweka
mkoa wetu katika hali nzuri,” alisema Dendego
Alisema Januari 14, aliitisha mkutano wa wadau wa elimu; viongozi wa
dini, wa halmashauri na mitaa kujadiliana namna ya kuinua kiwango cha
elimu mkoani humo.
“Tumeshapeana majukumu kila mtu katika eneo lake kuhamasisha kuhusu umuhimu wa elimu, hasa viongozi wa dini kwa waumini wao.
“Walimu nao wanatakiwa kufundisha kulingana na mazingira. Ubunifu
ukiongezeka katika ufundishaji, taratibu tunaweza kubadilisha upepo.
Naamini tukishirikiana suala hili litafanikiwa,” alisema.
Ofisa Elimu wa mkoa huo, Fatuma Kilimia alisema amedhamiria kuimarisha usimamizi ili kumaliza tatizo la udanganyifu.
“Tatizo hili linaonekana lilikuwapo. Hawa watoto walioanguka mtihani huu
mwaka 2014 walishika nafasi ya nane kitaifa kwenye mtihani wa darasa la
saba. Matokeo ni mabaya na hakuna namna ya kufanya zaidi ya kuimarisha
usimamizi na ufuatiliaji kwa walimu. Watoto hawawezi kufanya vizuri bila
kufundishwa,” alisema.
Katika orodha ya shule zenye matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2015, Mkoa wa Mtwara uliingiza shule 33.
Shule hizo zilikuwa kwenye mstari mwekundu ikimaanisha kuwa wanafunzi wake walifanya vibaya kupita kiasi kwenye mtihani huo.
Chingungwe, Naputa, Msimbati na Salama ni miongoni mwa shule za
sekondari zilizokuwa kwenye mstari mwekundu katika matokeo ya kidato cha
nne mwaka jana, Msimbati ikishika namba sita na Naputa namba 10.
Akizungumzia matokeo hayo, Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT),
Ezekiel Oluoch alisema mazingira magumu ya kazi mkoani Mtwara
yamechangia kwa kiasi kikubwa matokeo hayo.
Alisema shule nyingi zimekosa walimu kutokana na mazingira magumu na
Serikali imeshindwa kulifanyia kazi suala hilo ili kupata ufumbuzi.
“Tukubali kuwa Mtwara ni eneo lenye mazingira magumu ya kazi. Shule
hazina walimu na kwa bahati mbaya Serikali imekataa kutekeleza pendekezo
la CWT la kutoa posho kwa walimu walio katika mazingira magumu,”
alisema.
Oluoch alisema changamoto nyingine inayodumaza kiwango cha elimu Mtwara
ni kukithiri kwa mila na desturi, hivyo kuwazuia watoto kupata haki ya
elimu.
“Wenzetu kule unyago umepewa kipaumbele. Mzazi yuko radhi amzuie mtoto
kwenda shule akacheze, hapo ndipo tatizo linapotokea,” alisema Oluoch.
Post a Comment