0

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, amewaelekeza Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Clodwing Mtweve na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, George Lutengano, kuwasimamisha kazi watumishi watatu wa halmashauri hiyo kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha za Mpango wa Serikali wa Kuwezesha Shule za Sekondari nchini (SEDEP).
Pia amekataa kuweka jiwe la msingi katika nyumba za miradi ya SEDEP zilizopo Shule ya Sekondari Mwamanga na kufungua madarasa yaliyojengwa kupitia mradi huo yaliyopo kwenye Shule ya Sekondari Nyanguge.
Akizungumza juzi wakati wa ziara yake wilayani Magu, Mongella aliagiza kusimimishwa kazi kwa mweka hazina,  mchumi pamoja na mhandisi wa ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha za mradi wa SEDEP kwa madai haukufuata utaratibu.
“Miradi yote ya SEDEP Magu ina ukakasi, kuna maswali mengi katika miradi hii ambayo hayana majibu, muda wa utekelezaji wa mradi umekwisha lakini miradi mingi haijakamilika, hakuna majibu mazuri na inaonekana kuna fedha zimechezewa hapa.
“Mnanieleza eti fedha za SEDEP mlizipeleka katika ujenzi wa maabara lakini nasikia pia kuna fedha za afya na nyingine mlizokopa benki Sh milioni 302  bila kufuata utaratibu,” alisema Mongella.

Post a Comment

 
Top