Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassana ameishukuru
Serikali ya India kwa ufadhili wake wa miradi ya maji katika miji 17 nchi
ambayo inalenga kupunguza tatizo la maji kwa wananchi wengi nchini.
Ametoa
kauli hiyo Jijini Dar es Salaam katika hafla ya Maadhimisho ya miaka 68 ya Siku
ya Kitaifa ya Jamhuri ya India sherehe ambazo zimeambatana na Uzinduzi rasmi wa
majengo ya ofisi mpya ya Ubalozi wa India hapa nchini.
Makamu wa
Rais amesema ufadhili wa miradi ya Maji pamoja na miradi mingine unaofanywa na
Serikali ya India kwa Tanzania Bara na Zanzibar unadhihirisha wazi mahusiano
mazuri yaliyoasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere na Mahatma Gandhi wa India.
Makamu wa
Rais amesisitiza kuwa India ni moja ya washirika muhimu katika juhudi za
kuwaletea wananchi maendeleo na Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu
katika maeneo mengi ikiwemo ya kikanda na kimataifa kwa ajili ya manufaa ya
wananchi wa pande Mbili yaani Tanzania na India.
Makamu wa
Rais pia ameishukuru Serikali ya India kwa msaada wake wa shilingi milioni 500
alioutoa kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera ambao walikubwa na tetemeko la ardhi
mwaka jana.
Ameeleza
kuwa Mahusiano kati ya India na Tanzania yamekuwa na manufaa makubwa ambapo
idadi kubwa ya watanzania wanaenda kupata mafunzo mbalimbali nchini India hasa
Madaktari na wamekuwa msaada mkubwa katika kuokoa maisha ya Watanzania.
Pamoja na hayo, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa
salamu za rambirambi kwa Serikali ya India kufuatia ajali ya treni iliyotokea
katika Jimbo la Andhra Pradesh na kusababisha vifo vya watu 30 na kujeruhi
wengine.
Kwa
upande wake, Balozi wa India hapa nchini
Sandeep Arya amemhakikishia Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Serikali ya
India itaendelea kudumisha na kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo kwa ajili ya
manufaa ya wananchi wa pande zote Mbili.
Post a Comment