Katikati ya mwaka 2009, Brian Acton akiwa ni mtaalamu na msomi katika
masuala ya uhandisi wa programu za kompyuta (software engineer) ambaye
hakuna mtu aliyehitaji kumpa ajira katika kipindi hicho.
Licha ya kwamba
alikuwa ni mtu mwenye uzoefu mkubwa wa miaka mingi baada ya kufanya
kazi na makampuni makubwa ya kiteknolojia kama vile Yahoo na Apple
kabla hajaachana nao mwaka 2007, Brian alishindwa kabisa kupata nafasi
katika kampuni chipukizi zilizokuwa zikiingia kwenye soko la teknolojia
kwa wakati huo mojawapo ikiwa ni twitter mwezi Mei na baadae facebook
ukiwa mwezi Agosti mwaka 2009.
Mitandao yote miwili ya twitter na
facebook alimnyima kabisa Brian nafasi ya kuwa mmojawapo wa wahandisi
katika kampuni zao, kitu ambacho kilimfanya Brian kuumia sana lakini
hakukata tamaa pamoja na kukataliwa na mitandao hiyo.
Baada ya kukosa nafasi ya kujiunga katika makampuni makubwa mawili
aliyokuwa ameweka nia ya kufanya kazi nayo ambayo ni facebook na
twitter, Brian aliungana na mwenzake aliyekuwa wakifanya kazi pamoja
katika kampuni ya Yahoo hapo nyuma, Jan Koum, ambapo waliweza
kutengeneza “application” iliyoweza kutawala na kupata umaarufu mkubwa
duniani katika upande wa kutuma ujumbe mfupi (messaging). Ndio.
Huyu
ndiye Brian Acton mmoja wa waanzilishi na waendelezaji wa mtandao wa WhatsApp.
Mwaka 2014 facebook waliweza kurudi kwa Brian na Koum kuomba nafasi ya
kununua App hiyo ambapo waliweza kuwalipa kiasi cha $19 bilioni ikiwa ni
fedha taslimu na pia kwa njia ya kugawana hisa. Hii imemfanya Brian
kuwa na utajiri unaofikia 5.1 bilioni akiwa ni miongoni mwa mabilionea
wakubwa ndani ya taifa la Marekani na duniani kwa mujibu wa jarida la
Forbes hadi hivi sasa. Huku mshirika mwenzake Jan Koum akiwa na utajiri
unaofikia $8.2 bilioni hadi sasa.
“People want chat histories. They’re a permanent testimony of a relationship”
-Brian Acton
Nini unachotakiwa kujifunza kupitia ujumbe huu mfupi. Kuna mambo 4 ya kujifunza kupitia hali halisi aliyopitia Brian Acton:
1: Usivunjike Moyo Unapokataliwa.
Jambo muhimu unalopaswa kulifahamu katika suala la kutafuta mafanikio
ni kushikilia ndoto yako katika kila hali, haijalishi utapitia katika
kipindi au hali gani inayoweza kukufanya ushindwe kusimama na kuendelea
mbele. Unachopaswa kufahamu ili ndoto yako ifanikiwe inahitaji kiwango
cha furaha na amani ndani yako kila wakati, unaporuhusu kukata tamaa
unakuwa umeruhusu moyo wako kuvunjika na kushindwa kuendelea mbele na
huo utakuwa ni mwanzo wa kushindwa kufanikiwa kwako. Usiruhusu hali
yoyote ile kuja katika maisha yako na kukupotezea furaha na amani
ambavyo huwa kama sumaku na chaji ya kukusukuma katika kuelekea
mafanikio ya ndoto yako.
Kumbuka unapokata tamaa unaruhusu hali ya kushindwa, hebu fikiri kama
Brian Acton angekata tamaa baada ya kukataliwa kujiunga kwenye kampuni
ambazo ilikuwa ni ndoto ya maisha yake ingekuwaje? Lakini pamoja na
kukataliwa Brian hakukata tamaa akaamua kutumia hali hiyo kama
changamoto ya kumfanya afikiri zaidi kitu gani cha kufanya, na hatimaye
akaja na wazo jipya la kutengeneza application ya WhasApp akiwa pamoja
na mwenzake walioacha kazi pamoja Yahoo, Jan Koum.
2: Kukataliwa kunaweza kuwa ni fursa ya pili ya kufanikiwa kwako.
Hii inatusaidia kujua kumbe tunauwezo mkubwa ndani yetu. Najaribu
kufikiri kwa upande wa pili kama Brian Acton angekubaliwa kujiunga na
kampuni ya twitter au facebook leo hii tungepata wapi kuwasiliana kwa
haraka na kuweza kusaidiana kwa kupitia mtandao wa WhatsApp. Nataka
uelewe kuwa si kila mahali unapopita na kukataliwa ndio umefika mwisho
wa kutokufanikiwa kwako. Ni vyema zaidi wakati mwingine ujifunze
kutazama changamoto zinazokuijia au kukataliwa huko kama fursa ya
kufuata ndoto zako ulizonazo kwa muda mrefu. Brian alipata akili na
ubunifu ukaongezeka zaidi baada ya kukataliwa, hii ni wazi kukataliwa
huko kulikuwa ndio fursa ya yeye kufanikiwa na kufanya mambo makubwa
hapo badae.
Leo hii tunaona matajiri wengi zaidi ya Brian walipitia kukataliwa
ndio ukawa mwanzo wao wa kutoka na kufanikiwa kimaisha. Hebu mtazame
Jack Ma mmiliki wa Alibaba alikataliwa mara 30 katika kampuni mbalimbali
ikiwemo KFC na badae akakataliwa kujiunga na chuo kikuu cha Harvard
mara 10 na aliwahi kufeli mtihani wa chuo na kushindwa kuendelea mbele
kimasomo, lakini leo hii Jack Ma ni bilionea na tajiri mkubwa duniani.
Unachopaswa kufahamu ni kujifunza kupitia hali yoyote unayopitia sasa na
kuheshimu mawazo na nia ya dhati ya kufuata ndoto zako. Hupaswi
kushindana na watu wanaokudharau leo hii, huku ukweli ni kuwa una mtaji
mkubwa wa kuanzia uliomo ndani yako. Amua kusimama hadi uone matokeo
makubwa katika ndoto yako na hapo ndio mwanzo wa kuheshimiwa na
waliokukataa unaanza kuchipuka.
“Ukiongeza bidii na ufanisi kwa kile unachofanya amini waliokukataa watakutafuta.”
-Wilfred Tarimo
3: Tafuta mtu wa kukusaidia kuongeza nguvu ili kuleta matokeo makubwa.
Kikubwa unachotakiwa kufahamu ni kuwa unatakiwa kuelewa ni nani
unayeweza kuendana nae katika njia moja ili akusaidie kuleta matokeo
makubwa katika ndoto zako na kuishangaza dunia. Brian baada ya kukosa
nafasi ya kujiunga na kampuni ya twitter na facebook aliamua ndani ya
mwaka huo huo kumfuata rafiki yake waliyekuwa wakifanya kazi pamoja kwa
jina Jan Koum. Baada ya Brian kuungana na rafiki yake Koum ndio
walipoweza kuushangaza ulimwengu na kuja na “application” iliyopindua
ulimwengu katika upande wa ujumbe mfupi, WhatsApp.
Leo hii mamilioni ya watu duniani wanatumia mtandao wa WhatsApp
katika kuwasiliana hii ni kwa sababu ya watu ambao waliamua kutokukata
tamaa na kuamua kuzifuata ndoto zao hadi walipoona matokeo makubwa
yakitokea. Jiulize una ndoto gani uliyoikatia tamaa baada ya watu
kuinuka na kukuvunja moyo hata kuacha kuifuata ndoto yako tena? Nakusihi
usikate tamaa bali amua kuifuata na kuiishi ndoto yako hadi uone
matokeo makubwa yakitokea katika maisha yako. Jifunze kutafuta mtu
wakuambatana nae katika kufanikisha malengo na ndoto yako uliyonayo hasa
pale unapopitia katika wakati mgumu, kumbuka mmoja anaua makumi mkiwa
wawili mtaua maelfu.
4: Ukiongeza bidii na ufanisi kwa kile unachofanya amini waliokukataa watakutafuta.
Ndio. Hii ni wazi kabisa ukitaka wanaokudharau wakutafute hapo badae
ni wazi unahitaji uweke muelekeo wa kudumu (focus- concentration) kwenye
kile unachokifanya kama sehemu ya kutimiza ndoto zako. Usiruhusu
kutumia vibaya muda wako katika ushindani na magomvi au kuweka visa kwa
sababu umefanyiwa hila au ubaya wa aina yoyote, jifunze kuutazama ubaya
kwa hali chanya kwa ajili ya kukupa hatua mpya na kutengeneza misuli ya
mafanikio maishani mwako. Unahitaji kuushinda ubaya kwa wema ili
kuongeza hatua za mafanikio na spidi ya kufika kule unakoelekea. Jifunze
kuona hali ya kuchekwa na kudharaulika kama sehemu muhimu inayokuja
kwenye maisha yako kukusogeza (kuku-push) kwenye hatima njema ya
kufanikisha ndoto yako.
Facebook baada ya kuona WhatsApp inakuja kwa kasi na inaleta
ushindani mkubwa katika soko la teknolojia ya mitandao ya simu, hata
kuona hali ya kuja kupoteza watu wengi katika soko lake alilotawala kwa
kipindi kirefu, hali hii ilimfanya mmiliki wa facebook, Mark Zuckerberg
kuamua kurudi kwa Brian Acton yule waliyemkataa mwanzoni na kwa sasa
akitaka mwenyewe kufanya nae biashara. Nataka nikuambie bidii na ufanisi
wa Brian Acton baada ya kukataliwa ndio uliomfanya mmiliki wa facebook
kurudi nyuma na kuona kunahitajika busara ya kuungana na Brian kuliko
kupoteza watumiaji wengi wa mtandao wake. Ukiongeza bidii na ufanisi
utafanya makubwa na kusababisha waliokukataa hapo mwanzo kurudi kwako na
kuomba urafiki kwa upya. Kikubwa endelea kufanya unachofanya hadi ulete
matokeo yatakayokutambulisha katika dunia na kuwafanya adui zako kurudi
nyuma na kukuzingatia.
Post a Comment