Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imetoa sh. bilioni 1.4 kati ya sh.
bilioni 1.8 zilizotengwa katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya uendelezwaji wa
mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
Amesema
ujenzi wa hospitali hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ya mwaka 2015/2020 ya kuwa na zahanati katika kila kijiji, kituo cha afya
katika kila kata, hospitali katika wilaya na hospitali za rufaa kwa kila mkoa.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo, alipotembelea eneo la mtaa wa Wikichi inapojengwa
hospitali hiyo akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Njombe.
Amesema
lengo la ujenzi wa hospitali hiyo ni kuhakikisha mwananchi anaanza kupata
huduma za afya katika eneo lake na anapokuwa na tatizo kubwa ndipo atakwenda
hospitali ya wilaya na kisha hospitali ya rufaa ya mkoa.
Akitoa
taarifa ya ujenzi mradi wa hospitali hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe,
Jackson Saitabau amesema ujenzi wa hospitali hiyo ulianza katika eneo hilo
lenye ukubwa wa takribani ekari 70 katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, ambapo
kiasi cha sh. 953.705 zilitengwa kati yake sh. milioni 236.575 zilitumika kwa
ajili ya ulipaji wa fidia.
Amesema kuwa hadi sasa kazi ya ujenzi huo imekamilika kwa
asilimia 40 na mkandarasi ameshalipwa sh. milioni 892.963 sawa na asilimia 28
ya gharama za mradi na mtaalam mshauri amelipwa sh. milioni 51.50.
Post a Comment