0

MKUU wa Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, Chelestino Mofuga amemuagiza Mkuu wa Polisi wilaya hiyo, kumkamata mara moja mtumishi wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Ezekiel Felician kwa madai ya kuhamasisha wananchi wasiwatii viongozi wa wilaya hiyo na kumfukuza diwani.

Akizungumza katika mkutano wa matumizi bora ya ardhi, Mofuga alisema Felician amekuwa chanzo cha migogoro wilayani humo kwa kuwa amekuwa akihamasisha wananchi kugomea maagizo ya viongozi na badala yake amekuwa chanzo cha vurugu ndani ya wilaya hiyo.

Alitoa agizo hilo la kukamatwa kwa ofisa huyo wa ustawi wa jamii wakati akitatua mgogoro wa ardhi miongoni mwa wakazi wa wilaya hiyo.

Alisema kitendo cha wananchi kugomea mpango wa matumizi bora ya ardhi ni kosa ambalo wahusika wanapaswa kuchukuliwa hatua na pia mkuu huyo amepiga marufuku mikutano ya kimila ambayo inaitishwa bila ya vibali na kupinga maendeleo.

“Hakuna sheria ambayo inaruhusu wananchi kupinga viongozi, na pia kuna tabia ya kunyang’anyana wake zao, naagiza warudishwe kwa wahusika haraka sana,” alisema DC Mofuga na kuongeza “Waliong’oa ‘beacons’ (alama za mipaka) wakamatwe na kutozwa gharama za uharibifu ili iwe fundisho kwa wengine”alisema.

Akifafanua suala la unyang’anyi wa wake, alisema viongozi wa kimila wa kabila la datoga wameunda sheria za kutenga viongozi wa serikali pale ambapo hawaendani na matakwa yao na wale wanaofuata taratibu za serikali za matumizi bora ya ardhi wanatengwa kwa kunyang’anywa mke na ng’ombe.

Alisema mara nyingi wakishamnyang’anya mke wanamrudisha kwao na anakuwa chini ya usimamizi maalumu, hivyo imekuwa changamoto kubwa kwa ndoa nyingi kuvunjika na pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Post a Comment

 
Top