Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi ameonya
kwamba utaratibu uliotumika katika mchakato wa kumpata Mgombea wa CCM katika
kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Tanzania Mwaka 2015 ndio
utakautumika katika kumpata Mgombea wa Chama hicho upande wa Zanzibar ifikapo
uchaguzi wa mwaka 2020.
Amesema
utaratibu huo ndio silaha pekee itayosaidia kusafisha virusi vitakavyojaribu
kuibuka ndani ya chama hicho endapo yatatokea makundi
yatayoashiria kutaka kukiyumbisha Chama hicho utakapokaribia mchakato wa
Uchaguzi huo.
Balozi
Seif Ali Iddi ametoa onyo hilo hapo Nyumbani kwake Kama, wakati akizungumza na
Viongozi wa CCM kata ya Mtoni Jimbo la Temeke Mjini Dar es salaam ambao
wapo Zanzibar kwa mualiko wa wenyeji wao Kamati ya Ujirani Mwema ya Mkoa wa
Magharibi Unguja kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za Maadhimisho ya kutimia
Miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema
Chama cha Mapinduzi hakitawaonea haya wanachama wenye sura mbili na itakapobidi
italazimika chama hicho kusafisha taka taka hizo hasa katika kipindi
hichi cha mpito kuelekea kwenye uchaguzi ndani ya chama chenyewe.
Balozi
Seif amebainisha kusikitishwa kwake na Viongozi wa Chama hicho waliowahi
kudiriki kununua kadi za Chama na kuwapa baadhi ya Watu wengine wakiwemo
wapinzani ili wawachague katika kura za maoni na hatimae wapinzani
hao walitumia mwanya huo kuvuruga malengo na mikakati ya Chama cha Mapinduzi.
Mjumbe
huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliwakumbusha Viongozi na wanachama wa
Chama cha Mapinduzi walazimike kufanya kazi ya ziada
katika kuwabaini wanafiki hao katika kutoa maamuzi yao wakati wa uchaguzi
wa ndani ya Chama.
Akizungumzia
Maadhimisho ya sherehe za kutimia Miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Seif
amesisitiza kwamba masuala hayo yataendelea kuwa na umuhimu kwa Wazanzibari na
Watanzania wote katika kujikumbusha juu ya utawala wa Kikolini uliong’olewa na waasisi wa
Mapinduzi hayo Mwaka 1964.
Amewahakikishia
Viongozi na wanachama hao wa CCM kwamba yale yote yaliyoasisiwa na Viongozi wa
Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 yataendelea kutekelezwa daima.
Post a Comment