0

MTU mmoja Mkazi wa Kijiji cha Kanyelele , Safari Bungate (51) ameuawa na kundi la watu waliojichukulia sheria mkononi kwa kumpiga mtu huyo mawe na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kuiba kuku katika nyumba ya mmiliki wa kuku, Tetema Mathias (40), mkulima na mkazi wa kijiji cha Kanyelele, kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu, Kamishina, Ahmed Msangi amesema tukio hilo limetokea Januari 26 mwaka huu majira ya saa nne usiku katika kijiji cha Kanyelele tarafa ya Usagara Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.
Taarifa hiyo inadaiwa kuwa mwenye nyumba, Tetema Mathias akiwa amelala na familia yake, alikuja mtu/marehemu akaingia ndani kupitia dirishani na kuiba kuku mmoja, ndipo wakati alipokuwa anataka kuondoka Mathias alimuona na kuanza kupiga yowe ya mwizi akiomba majirani waje wamsaidie kumkamata huku akimkimbiza barabarani.
Hata hivyo taarifa ilidai kuwa watu/ majirani waliamka na kufanikiwa kumkamata marehemu akiwa na kuku amemshikilia kisha wakaanza kumpiga kwa mawe na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake kitendo kilichosababisha mtu/ marehemu huyo kupoteza fahamu na baada ya muda mchache alifariki dunia. 
Taarifa ya Kamanda Msangi amesema raia wema walitoa taarifa polisi ndipo askari walifika eneo la tukio na kukuta mtuhumiwa wa wizi akiwa tayari amefariki dunia na mwili wa marehemu tayari umefanyiwa uchunguzi na daktari na kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.
Jeshi la Polisi linamshikilia Tetema Mathias kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Naibu, Kamishina Msangi ametoa wito kwa wakazi wa Jiji na Mkoa wa Mwanza, akiwataka kuacha tabia ya kujichulia sheria mkononi kwani ni kosa la jinai, aidha anawataka wananchi pindi wanapomkamata mhalifu wamfikishe katika vyombo vya sheria ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.
Chanzo-Michuzi blog

Post a Comment

 
Top