Meneja wa Uwezo Tanzania, Zaida Mgalla
UTAFITI uliofanywa na asasi ya Twaweza, juu ya uhusiano kati ya lishe na
matokeo ya kujifunza, umebaini kuwa wenye utapiamlo wanafeli zaidi
kusoma masomo ya Kiingereza na Hisabati kuliko wale ambao hawana
utapiamlo.
"Uhusiano ni mkubwa kati ya matokeo ya kujifunza na utapiamlo, Twaweza
inatoa mwito kwa wazazi na shule kuhakikisha watoto wanapata chakula
shuleni," ulisema utafiti huo, ambao ulitangazwa jana na Twaweza kupitia
programu ya Uwezo.
Takwimu za utafiti zilikusanywa kati ya Oktoba na Desemba 2015 kutoka
kwa watoto 197,451 na kaya 68,588.
Utafiti huo unaonesha kuwa uhusiano kati ya matokeo ya watoto ya
kujifunza na utapiamlo, miongoni mwa watoto wenye miaka 10 mpaka 14 kwa
upande wa somo la Kingereza, uwezo wa kusoma hadithi ya Kiingereza ya
darasa la 2 ilitofautiana.
Kiwango kilionesha kuwa watoto wenye utapiamlo, walifaulu kidogo wakati
wale ambao hawana utapiamlo walifaulu zaidi.
Asilimia 17.9 ya watoto wenye utapiamlo walifaulu, wastani wa asilimia
16.4 ya watoto wenye utapiamlo wa wastani walifaulu, lakini watoto wasio
na utapiamlo asilimia 25.8 walifaulu kusoma hadithi ya kiingerza ya
darasa la pili.
Kwa upande wa somo la Kiswahili, uwezo wa kusoma hadithi ya Kiswahili ya
kiwango cha darasa la 2, watoto wenye utapiamlo (asilimia 46.3
walifaulu), watoto wenye utapiamlo wa wastani ( asilimia 51.3 walifaulu)
na watoto wasio na utapiamlo ( asilimia 65.8 walifaulu).
Ripoti inaonesha kuwa katika somo la Hisabati, uwezo wa kufanya hesabu
za kuzidisha za kiwango cha darasa la 2, watoto wenye utapiamlo (
asilimia 35.5 walifaulu), watoto wenye utapiamlo wa wastani ( asilimia
37.7 walifaulu) na watoto wasio na utapiamlo asilimia 53.4 walifaulu.
Matokeo haya yalitolewa jana na Twaweza katika hafla iliyofanyika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam. Hafla hiyo ni sehemu ya mfululizo wa semina za
Jielimishe, zinazofanyika kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu na Twaweza.
Meneja wa Uwezo Tanzania, Zaida Mgalla, alisema hali ya lishe ya
watoto, ina madhara kwenye kusoma Kiingereza ukilinganisha na Kiswahili
na Hisabati.
Habari njema ni kwamba suala hili linaweza kujadiliwa, na watoto
wanaweza kupatiwa chakula shuleni. Utoaji wa chakula shuleni unaweza
ukawa njia mojawapo ya kuwapa motisha wanafunzi kuhudhuria zaidi
shuleni.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema uwezo wa watoto
kufanya vizuri shuleni, unaathiriwa na jinsi wanavyopata lishe nzuri.
Aliongeza kuwa katika awamu hii ya elimu bila malipo ya ada, suala la
utoaji wa chakula shuleni limeachwa njia panda.
"Halijaainishwa kwenye fedha za ruzuku zinazotumwa moja kwa moja
shuleni na serikali. Wazazi nao wameacha kutoa michango shuleni,
kutokana na matamko rasmi ya kufuta michango yote mashuleni. Je, suala
la michango ya wazazi kwa ajili ya chakula cha watoto wao wakiwa shuleni
bado halizungumziki," alisema Eyakuze.
Twaweza ilisema kuwa takwimu zilizokusanywa, zinaonesha kuwa kitaifa
asilimia 4 ya watoto wenye umri chini ya miaka 5, asilimia 5.6 ya watoto
wenye miaka kati ya 5 na 9 na asilimia 5.7 ya watoto wenye miaka kati
ya 10 hadi 14 wana utapiamlo.
Utafiti huo ulifafanua kuwa hata hivyo kuna utofauti mkubwa kiwilaya,
kwani kwa Songea Mjini asilimia 23.9 ya watoto walio chini ya miaka 5
wana utapiamlo, ukilinganisha na asilimia 0.3 ya watoto wa wilaya ya
Tabora Mjini na Musoma Mjini.
Pia utafiti umebaini kuwa wastani, asilimia 50 ya kaya zinamudu milo
mitatu kwa siku na matokeo ya utafiti, yanaonesha kuwa baadhi ya wilaya
zina zaidi ya asilimia 85 ya kaya zinazomudu milo mitatu kwa siku.
Wilaya hizo ni Mbulu asilimia 97.6, Kishapu asilimia 88.2, Mafinga Mjin
asilimia 88, Tunduma asilimia 86.4, Moshi Mjini asilimia 86.
Katika wilaya nyingine, kaya chini ya asilimia 40 ndizo zinazomudu milo
mitatu kwa siku nazo ni Masasi asilimia 38.6, Tandahimba asilimia 35.5,
Mtwara Vijijini asilimia 27.6 na Nanyumbu – asilimia 23.1.
Kitaifa, ni shule moja tu kati ya tano inayotoa huduma ya chakula cha
mchana shuleni (asilimia 23). Kwa mkoa wa Kilimanjaro, asilimia 79 ya
shule zinatoa chakula cha mchana, lakini katika mkoa wa Geita, ni
asilimia 5 tu ya shule zinazomudu chakula cha mchana kwa watoto.

Post a Comment