RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein
amesema kuwa uchumi wa Zanzibar umezidi kumeimarika sambamba na Serikali
kufanikiwa kuongeza kiwango cha makusanyo ya kodi ambapo kwa kipindi cha
Januari hadi Novemba, mwaka 2016
jumla ya sh. bilioni 441.3 zimekusanywa kutoka vyanzo vya ndani.
Katika risala yake ya kuukaribisha mwaka mpya 2017 aliyoitoa leo kupitia vyombo vya habari, Ikulu mjini Zanzibar Dkt. Shein amesema kuwa kwa kipindi kama hiki mwaka
2015 Serikali ilikusanya Sh. bilioni 336.6 ikimaanisha kwamba miezi kumi ya
mwanzo ya mwaka 2016, mapato yameongezeka kwa Sh. bilioni 104.7 sawa na ukuaji wa asilimia 31.1.
Amesema kuwa sambamba na mafanikio hayo, washirika wa
maendeleo wamethamini kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya kuwaletea maendeleo
wananchi ambapo katika kuthibitisha imani yao kwa Zanzibar, Serikali imepokea
jumla ya Sh.bilioni 54.53 kutoka kwa
Washirika wa Maendeleo kati ya Januari hadi Oktoba 2016.
Aidha, Dkt. Shein amesisitiza kauli yake aliyoitoa Disemba 10, 2016 katika
maadhimisho ya siku ya Maadili kwenye viwanja vya bustani ya Victoria ya
kuwataka viongozi wa umma wanaohusika
kujaza fomu kwa kuzingatia maelekezo yaliotolewa kwenye fomu hio na
waepuke kutoa taarifa zisizo za kweli kwani kufanya hivyo ni kitendo cha
kuvunja maadili ya uongozi.
Akieleza juu ya amani na utulivu katika
kusherehekea mwaka mpya, Dk.
Shein amesema Serikali haitosita kumchukulia hatua mtu yoyote au
kikundi cha watu kitakachofanya vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wa
wananchi na mali zao pamoja na
wageni wanaoitembelea Zanzibar.
Dk. Shein ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi wote
kushirikiana kukomesha vitendo
vya udhalilishaji, amesema ufumbuzi wa changamoto hiyo unahitaji mchango wa
kila mmoja na sio Serikali pekee.
Pia, Dk. Shein ameendelea kutoa wito kwa
wananchi kushiriki katika maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi matukufu ya
Zanzibar, yanayotanguliwa na shamra shamra mbali mbali za uzinduzi wa miradi wa
miradi na uwekaji wa mawe ya msingi.
Post a Comment