Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli,
leo tarehe 22 Desemba, 2016 amemteua Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe.
Jaji Semistocles Kaijage kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC).
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza
kuwa Mhe. Jaji Semistocles Kaijage ameteuliwa kuongoza Tume hiyo
kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia tarehe 20 Desemba, 2016.
Mhe. Jaji Semistocles Kaijage anachukua nafasi ya Mhe. Jaji Mstaafu
Damiani Lubuva ambae muda wake wa kuwa Mwenyekiti umemalizika rasmi
mnamo tarehe 19 Desemba, 2016.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhe. Jaji Mstaafu Hamid Mahamoud
Hamid kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa
kipindi kingine cha miaka mitano kuanzia tarehe 20 Desemba, 2016.
Mhe. Jaji Mstaafu Hamid Mahamoud Hamid alikuwa Makamu Mwenyekiti wa NEC
na amemaliza kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano mnamo tarehe 19
Desemba, 2016.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli pia amemteua Jaji Mstaafu wa Mahakama
ya Rufaa, Mhe. Jaji Harold Reginald Nsekela kuwa Kamishna wa Maadili
katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kipindi cha miaka
mitano kuanzia tarehe 20 Desemba, 2016.
Mhe. Jaji Mstaafu Nsekela anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Jaji
Mstaafu Salome S. Kaganda ambae amestaafu mnamo tarehe 10 Desemba, 2016.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amewateua Majaji wanne wa
Mahakama Kuu kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani kuanzia leo tarehe 22
Desemba, 2016 kama ifuatavyo:-
i) Mhe. Jaji Dkt. Gerald Ndika
ii) Mhe. Jaji Jackobs Mwambegele
iii) Mhe. Jaji Rehema Kiwanga Mkuye
iv) Mhe. Jaji Sivangilwe Sikalalilwa Mwangesi
Wateule wote waliotajwa katika taarifa hii wataapishwa kesho Ijumaa,
tarehe 23 Desemba, 2016 saa 3:00 asubuhi Ikulu Jijini
Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Desemba, 2016

Post a Comment