Kutokana na maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kupungua kwa asilimia
50 duniani kote na kupelekea watu milioni 2.1 tu kuambukizwa Virusi vya
Ukimwi katika mwaka 2015,kumeibua matumaini mapya ya kuwa na watu wasio
na maambukizi ya virusi vya Ukimwi ifikapo mwaka 2030.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini Tanzania
(TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko aliwaambia waandishi wa habari jana Jijini
Dar es Salaam kuwa, nchini Tanzania maambukizi mapya ya virusi vya
Ukimwi nayo yameshuka kwa asilimia 20 ambapo watu 54,000 wameambukizwa
virusi hivyo kwa mwaka 2015 pekee.
Dkt. Maboko alisema, Ukimwi bado ni janga kubwa duniani na taifa kwa
ujumla huku akitaja kundi la wanawake kuwa ndilo lina kiwango cha juu
cha maambukizi ya VVU huku mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya ukiwa na
kiwango cha juu cha maambukizi hayo kitaifa.
Aidha, alisema serikali imejiwekea mikakati kuhakikisha kuwa
waliogundulika kuwa wameathirika wanaanzishiwa dawa, kuhimiza matumizi
ya mpira wa kiume, kupunguza maambukizi mapya kwa asilimia 29 na kutoa
elimu kwa wanawake wanaojihusisha na ngono, kupunguza maambukizi ya
virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Post a Comment