Kauli ya Kingunge imekuja siku moja baada Rais John Magufuli kumteua
Jaji Themistocles Kaijage kuwa mwenyekiti mpya wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) baada ya Jaji Damian Lubuva kufikia muda wake wa
kustaafu.
Kwa muda mrefu, NEC imekuwa ikilalamikiwa na vyama vya upinzani kwa
kutokuwa huru kwa sababu ya uongozi wake wote huteuliwa na Rais ambaye
pia ni mwenyekiti wa CCM, huku sheria zikikataza matokeo ya nafasi ya
urais kupingwa mahakamani.
Mbali na mwenyekiti kuteuliwa na Rais, wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo
ni wakurugenzi wa wilaya ambao pia huteuliwa na Rais kwa kuwa NEC haina
wafanyakazi wake kote nchini.
Akizungumza katika mkutano wa kuwafariji vijana waliokamatwa na Jeshi la
Polisi na kushtakiwa kwa makosa yaliyohusu Uchaguzi Mkuu uliopita,
uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Kingunge aliwatia moyo vijana
hao, akisema hakuna ushindi unaopatikana bila kupambana.
Kingunge, aliyetumia muda mrefu kueleza historia ya maisha yake katika
siasa na jinsi alivyopambana katika harakati za kudai uhuru, alisema
hali ya sasa ni mbaya kuliko wakati wa wakoloni wa Kiingereza ambao
walikujwa wakali, kwa sababu CCM haifuati Katiba wala sheria.
“Yako mambo ambayo itabidi tujitahidi yaamuliwe sasa kabla ya 2020.
Mambo hayo makubwa kwanza ni tume huru (ya uchaguzi). Suala hilo lazima
lizungumzwe sasa, hatuwezi kwenda 2020 na tume ya sasa na Katiba ya
mwaka 1977. Tukienda hivyo sahau habari ya upinzani kushinda uchaguzi,”
alisema.
Kingunge ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo
ya waziri anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi) na mkuu wa mkoa alisema, “(Pia) Sheria inayohusu matokeo ya
uchaguzi wa Rais kuhojiwa. Hivi sasa sheria inasema matokeo ya uchaguzi
wa Rais hayahojiwi mahakamani. Lazima hilo suala lipate jibu sasa. Kwa
hiyo Katiba na sheria iseme, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanaweza
kuhojiwa mahakamani. Tusipokuwa na hilo, tutakuwa na matatizo makubwa
sana.”
Alisema pamoja na kwamba Chadema inapendwa na wananchi wengi na Edward
Lowasa aliyegombea urais kwa tiketi chama hicho, anapendwa, bado ni
vigumu kushinda kwa sababu mfumo uliopo sasa.
“Tufanye yoyote, lakini tuhakikishe, ama tunapata Katiba Mpya au
vipengele hivi vya sheria vinafanyiwa marekebisho. Kwa maoni yangu,
kundi hili lililo madarakani bila shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi,
halitataka mabadiliko,” alisema.
Alisema enzi zao walifanikiwa kupata uhuru kwa sababu walijitolea kwa
nguvu na wengine, na yeye akiwamo, waliacha kazi za mishahara mikubwa na
kujiunga na Tanu kupigania uhuru.
“Tulifanikiwa kupata uhuru kwa sababu walijitoa mhanga. Wengi tu
waliacha kazi, mtu anamaliza chuo kikuu anasema sitaki kazi anaingia
Tanu kusaidia. Kwa hiyo tukawa na jeshi kubwa la vijana waliohakikisha
nchi inapata uhuru,” alisema.
“Ninyi mnapambana katika mazingira magumu na wazee wenzenu walipambana
katika mazingira hayo. Haikuwa rahisi. Wapo wengi walitusaliti, wengine
hawakufanya lolote. Baba yangu tuligombana, nilipoacha kazi kwenda
kuitumikia Tanu. Miezi sita hatukuzungumza.”
Akizungumza mkutano huo, Lowassa, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya
Chadema, aliwatia moyo vijana walioshtakiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015, akisema bado jeshi kubwa la vijana linahitajika.
“Yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo. Si haki kusema
unakwenda mahali pengine, mwenzako amepasafisha, safisha pa kwako.
Nimefurahia moyo huo. Kama alivyosema Ngombale, tunataka jeshi kubwa
zaidi, watu wengi zaidi,” alisema Lowassa.
Post a Comment