Habari
zilizotufikia kutoka Hospitali ya Tumaini zinasema kwamba Profesa Idris
Ali Mtulia amefariki dunia usiku wa kuamkia leo akiwa usingizini.
Afisa
mmoja wa Hospitali ya Tumaini iliyopo jijini Dar es Salaam
alithibitisha kutokea kwa kifo hicho lakini hakueleza kwa undani
alipopigiwa simu na mwanahabari wetu.
“Ni
kweli amefariki dunia akiwa usingizini,” alisema bila kufafanua na
kukata simu huku baadhi ya wagonjwa wakisema kuwa walikuwa na ahadi ya
kuonana naye leo katika hospitali hiyo ili awatibu.
Prof. Mtulia alikuwa daktari bingwa wa kwanza wa moyo nchini na wataalamu wenzake wakampachika jina la utani la Mchawi wa Moyo.
Enzi ya uhai wake, aliwahi kuwa daktari wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, mzee Ally Hassan Mwinyi akiwa madarakani.
Prof.
Mtulia pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Mbunge wa
Jimbo la Rufiji, aliwahi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)
kuanzia mwaka 2002 hadi 2007. Ameacha mjane na watoto sita.