Wakili wa Serikali, Patrick Mwita amemuomba radhi Hakimu Mkazi Mkuu wa
Kisutu kwa kushindwa kutekeleza amri ya kumkamata mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anayekabiliwa na kesi ya uchochezi
pamoja na wahariri wa gazeti la Mawio.
Wakili Mwita alifanya hivyo jana baada ya hakimu huyo, Thomas Simba
kumuhoji sababu za kushindwa kutekeleza amri hiyo wakati hati ya
kumkamata ilitolewa Novemba 3, 2016 na wakili huyo kuisaini.
“Kwa nini hamkumkamata” Si mlikuwa na wajibu wa kumkamata? Mnamuogopa?” alihoji hakimu huyo.
Hata hivyo, pamoja na kuomba radhi hiyo mahakama imechukua hati ya
kusafiria ya Lissu ili kudhibiti safari zake nje ya nchi kwa kuwa
amekuwa akisafiri bila kuitaarifu mahakama.
Katika kesi hiyo, Lissu na watu wengine watatu wameshtakiwa kwa makosa
matano ya uchocheza kutokana na habari iliyochapishwa na gazeti la Mawio
kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar.
Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 28, 2016 na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.
Kabla ya uamuzi huo, Wakili Mwita alisema jana ilikuwa siku ya kesi hiyo kutajwa na kwamba upelelezi unakaribia kukamilika.
Kuhusu madai ya kudharau mahakama Wakili Peter Kibatala anayemwakilisha
Lissu aliiambia mahakama kuwa mteja wake yupo mahakamani, hivyo ametii
amri ya mahakama na kwamba jukumu la dhamana ni kuhakikisha mshtakiwa
anakuwapo mahakamani wakati wa kesi yake na kwamba uwepo wake ni kutii
masharti ya dhamana.
Hata hivyo, Wakili Mwita alidai kuwa kitendo cha Lissu kutofika
mahakamani mara mbili mfululizo ni kama kuonyesha dharau kwa mahakama
hiyo.
Mwita alidai kuwa Lissu ni mwanataaluma wa sheria na anafahamu taratibu
za kufuatwa kama hafiki mahakamani na kwamba mdhamini si mbadala wa
mshtakiwa mahakamani.
“Alipaswa kuandika barua kuitaarifu mahakama hii kama wakili kuwa ana
kesi ya uchaguzi anayoiendesha Bunda na kuambatanisha na samansi ama
orodha ya kesi. Tunaomba mahakama iheshimiwe na jukumu la kumfutia
dhamana ama kutokumfutia dhamana Lissu bado lipo mikononi mwako
mheshimiwa,” alieleza wakili huyo wa Serikali.
Akizungumzia hoja hizo, Hakimu Simba alisema Lissu ni wakili maarufu,
msomi na anajua taratibu zote za mahakama, lakini wadhamini wake
wanababaika, hivyo alimtaka aeleze sababu za kwenda Ujerumani bila kutoa
taarifa mahakamani.
Lissu alijibu kuwa hakuwa na nia ya kuidharau mahakama, wala kuikimbia
kesi inayomkabili bali alikwenda Ujerumani katika mazingira ya dharura.
Hakimu Simba alimwambia mahakama inafahamu kesi za uchaguzi na maelekezo
yake, hivyo ikamuuliza sababu za kutotoa taarifa wakati alipokwenda
kushughulikia kesi ya Bunda
“Nilipopata taarifa ya kwenda kuiendesha kesi hiyo ilikuwa ni siku moja
baada ya kutoka nchini Ujerumani na kwamba niliandika barua ya
kuitaarifu mahakama na nilituma iletwe mahakamani kupitia wasaidizi
wangu,” alisema Lissu.
Lakini Hakimu Simba alisema: “Hakuna barua iliyotufikia. Usituingize
katika migogoro kutokana na nafasi yako katika jamii ya mwanasheria.
Hatukuogopi labda upande wa mashtaka ndio wamekuogopa.
“Tunataka kufuata mfumo, hatutakuogopa na wala hatutakuonea. Hapa naona
upande wa mashtaka wanapiga blaa blaa, tuelewane tunaichukua hati yako
ya kusafiria ili ukitaka kusafiri tujue.”
Post a Comment