0

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amekiri kuwepo kwa askari polisi wapya 297 katika Idara ya Uhamiaji ambao hawakuwa wamelipwa malipo yao huku akiilaumu idara hiyo kwa kutowatendea haki huku wakifanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini katika kipindi cha miezi minne.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na uongozi wa idara hiyo alipofanya ziara ili kujua changamoto mbalimbali zinazoikabili eneo hilo na kuwataka wanaohusika katika suala hilo kuonana naye leo saa mbili asubuhi.

“Juzi niliulizwa swali bungeni la vijana wapya waliokuwa na ajira mpya kutolipwa malipo kwa wakati, nilipofuatilia nikagundua tatizo lilikuwa kwetu, niliongea na Waziri wa Utumishi na akanieleza kuwa sisi hatukupeleka majina,” alisema Mwigulu huku akimtaka anayehusika kutoa maelezo.

Alimtaka Ofisa Utawala wa Idara hiyo, Mulegi Majogoro kujiuliza kama anaona kwa miezi yote minne ni haki kutokufanya yanayostahili au ilikuwa ni kazi nzito sana ili askari hao kupatiwa malipo yao.

Akijitetea, Mulegi alisema askari hao waliripoti Agosti 9, 2016 na walipokewa wakiwa na barua zao na vyeti vya elimu ambavyo vilipopelekwa Utumishi vilibainika kuwa na kasoro ikiwamo kasoro za herufi za majina katika vyeti vya kuzaliwa na vya taaluma pamoja na miaka ya kuzaliwa, zikitakiwa kufanyiwa marekebisho.

“Wewe unavyoona kuanzia mwezi wa kwanza hadi wa nne uliona kurekebisha suala hilo ni kazi nzito sana,” alihoji Mwigulu huku ofisa huyo akijitetea kuwa idara hiyo inakabiliwa na changamoto ya intaneti pamoja na kukatika kwa umeme.

Post a Comment

 
Top