Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicholas Mgaya
****
SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) limeunga mkono utaratibu wa
serikali wa kuhakiki vyeti vya watumishi wa umma na kutaka utaratibu huo
ufanyike pia kwenye sekta binafsi kama alivyoshauri Mwenyekiti wa Bodi
ya Chuo Kikuu cha Iringa (Uol), Askofu Dk Owdenburg Mdegella.
Pamoja na shirikisho hilo, pia baadhi ya vyama vya wafanyakazi navyo
vimeunga mkono utaratibu huo na kuitaka serikali ihakikishe inaondoa
watumishi wote wanaotumia vyeti feki ili kutoa nafasi kwa wasomi wengi
wanaohangaika mtaani kwa kukosa ajira.
Akizungumza na gazeti la Habarileo jana, Katibu Mkuu wa shirikisho hilo,
Nicholaus Mgaya alisema uhakiki huo utasaidia kuondoa watumishi wengi
wasiowajibika kwa kukosa sifa na kuhakikisha wale wenye sifa ndio
wanapata ajira.
“Tunaomba huu uwe utaratibu wa nchi nzima, maeneo yote yaguswe na
uhakiki huu kwa sababu ukweli uko wazi kwa sasa kuna watanzania wengi
tena wasomi wa hali ya juu hawana ajira lakini nafasi zao zimezibwa na
watu wasi na sifa,” alisisitiza Mgaya.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao
na Mawasiliano Tanzania (Tewuta), Yunus Ndaro alisema vyama vya
wafanyakazi vinaunga mkono hatua hiyo ya serikali kwani itasaidia
kurejesha heshima ya ajira nchini.
Alisema sekta binafsi pia ni sehemu ya Tanzania na inajiendesha pia kwa
kufuata Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Mwaka 2004, hivyo nayo inapaswa
kuhakikiwa ili kuhakikisha inafuata misingi, kanuni na sheria za nchi.
“Mfano zipo kampuni nyingi za simu baadhi yake zikiwa binafsi zinaingiza
wafanyakazi wageni kutoka nje ya nchi, wengi wakiwa hawana sifa,
kupitia uhakiki huu haya yote yatavumbuliwa,” alisisitiza Ndaro.
Hata hivyo, alisema endapo serikali isipochukua uamuzi wa kuhakiki na
sekta binafsi wale watumishi wa umma wote wadanganyifu watakaobainika
kuwa na vyeti feki watakimbilia sekta binafsi hali itakayoendeleza zaidi
tatizo la ajira.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa Kujitegemea, Emmanuel Makene alisema
uhakiki wa vyeti hivyo, unafanyika kwa mujibu wa sheria kutokana na
ukweli kuwa sheria ya ajira inakataza mfanyakazi kughushi cheti.
“Hapa hakuna mtu wa kulaumiwa, serikali inatekeleza sheria kama
inavyotaka, kifungu cha 338 na 342 cha Sheria ya Ajina na Mahusiano kiko
wazi ni kosa la jinai kughushi. Na ni kweli watu wanaofanya hivi wapo
lazima watafutwe na kuchukuliwa hatua,” alisisitiza Makene.
Wakati serikali ikiendelea na uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa
serikali, hivi karibuni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Iringa
(UOI), Askofu Dk Owdenburg Mdegella pamoja na kuipongeza serikali kwa
kuanzisha utaratibu huo, pia ameomba ufanyike hadi sekta binafsi ili
kupunguza ongezeko la vyeti bandia.
Chanzo-Habarileo
Post a Comment