Kikosi Kazi cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam cha kuzuia wizi wa
magari kimeendelea na kazi ya kudhibiti vitendo hivyo kwa kumkamata
Padri wa Kanisa Katoliki Sumbawanga Demestrious Apolinary kwa tuhuma za
kuhusika na ununuzi wa gari ya wizi.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda Simon Sirro
amesema mnamo Novemba, 11 baada ya padri huyo kununua gari aina ya
Toyota L/cruiser T616 DCH mali ya Joseph Kayawaya lililoripotiwa kuibiwa
Dar es Salaam na nyaraka za kughushi na kuuzwa jijini Arusha.
Amesema padri huyo anafanyiwa mahojiano na kwamba upelelezi
utakapokamilika atapelekwa mahakamani ili kuona kama ni mnunuzi asiye na
hatia au alishiriki kwa namna moja au nyingine katika wizi huo.
Kamanda Sirro amesema pia Jeshi la Polisi linashikilia watuhumiwa
wengine wanne aliowataja kwa majina ya Aman Dickson, Exaud Martin,
Rashid Haruna na Mzee Nasibu kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa magari
katika matukio mawili tofauti.
Katika tukio lingine, Kamanda Sirro amesema Jeshi la Polisi linashikilia
majambazi watano na vifaa mbalimbali walivyopora maeneo ya Tuwangoma
mtaa wa Masaki, Mbagala.
Post a Comment