0


MBEYA City Council FC imeutumia vizuri Uwanja wa nyumbani, Sokoine mjini Mbeya baada ya kuwafunga mabingwa watetezi, Yanga mabao 2-1.

Ushindi huo wa kwaza kwa Mbeya dhidi ya Yanga tangu wapande Ligi Kuu, unaifanya MCC ifikishe pointi 19 baada ya kucheza mechi 14, wakati Yanga inabaki na pointi zake 27 za mechi 13.

Mbeya City waliuanza vizuri mchezo na kufanikiwa kumaliza kipindi cha kwanza wanaongoza kwa mabao 2-1.

Beki wa kushoto wa MCC, Hassan Mwasapili aliifungia timu yake bao la kwanza dakika ya sita baada ya kumtungua vizuri kipa wa Yanga, Deo Munishi ‘Dida’ kwa shuti la mbali la mpira wa adhabu.

Nahodha Kenny Ally akaifungia Mbeya City bao la pili dakika ya 36 kwa shuti la mbali pia baada ya kuanzishiwa mpira wa adhabu na beki wa kulia Haruna Shamte, aliyechezewa rafu na beki wa Yanga, Hassan Kessy.

Bao hilo lilizua utata baada ya wachezaji wa Yanga kumfuata refa Rajab Mrope wa Ruvuma kulikubali, kulikataa baada ya kuzongwa na wachezaji na Yanga na kulikubali tena baada ya majadiliano na wasaidizi wake.

Lakini kilichoonekana ni wachezaji wa Yanga walikuwa wamezubaa hawakujipanga na Shamte akatumia mwanya huo kumuanzishia mfungaji haraka, ambaye aliunganishia shuti nyavuni.

Wachezaji wa Mbeya City wakamvamia refa huyo na wakati huo huo mashabiki wao waliingia uwanjani na wengine walikuwa wakirusha chupa za maji kutoka jukwaani, hadi amani ikachafuka uwanjani.

Wakati huo huo refa huyo alikuwa akizongwa na wachezaji wa Mbeya City na ghafla akageuka na kulibariki hilo, hivyo mchezo kuendelea.

Mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma akaifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 45 baada ya kuwatoka mabeki wa Mbeya City na kumtungua kipa Mmalawi Owen Chaima.

Kipindi cha pili, kocha Mholanzi wa Yanga, Hans van der Pluijm alianza kumpumzisha kiungo wa ulinzi, Mbuyu Twite na kumuingiza Mzimbabwe, Thabani Kamusoko kabla ya baadaye kumtoa winga Deus Kaseke na kumuingiza Geoffrey Mwashiuya.

Katika kipindi hicho cha pili, Kocha Mmalawi wa Mbeya City alionekana kubadilisha mbinu na kuamua kucheza mchezo wa kujihami kuulinda ushindi wao, hivyo kuwapa kazi Yanga ya kuupasua ukuta wao.

Kinara wa mabao wa Yanga, Amissi Joselyn Tambwe hakuwa katika siku nzuri leo baada ya kukosa bao wazi dakika ya 64 akiunganishia nje kwa kichwa krosi ya Ngoma.

Mbeya City waliendelea kucheza kwa kujihami hukui wakipeleka mashambulizi ya kushitukiza langoni mwa Yanga hadi kipyenga cha mwisho.

Wachezaji wa Yanga wakamvaa tena refa wakidai amemaliza mchezo kabla ya muda, hivyo kusababisha atolewe uwanjani kwa msaada wa Jeshi la Polisi.

Kikosi cha Mbeya City kilikuwa; Owen Chaima, Haruna Shamte, Hassan Mwasapili, Sankhani Mkandawile, Rajab Zahir, Tumba Lui, Raphael Daud, Kenny Ally, Ditram Nchimbi, Hamedy Murutabose/Omary Ramadhani dk18 na Joseph Mahundi/Issa Nelson dk90+.

Yanga; Deo Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy, Mwinyi Haji Mngwali, Andrew Vincent, Vincent Bossou, Mbuyu Twite/Thabani Kamusoko dk46, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe/Obrey Chirwa dk68, Donald Ngoma na Deus Kaseke/Geoffrey Mwashiuya dk51.

Post a Comment

 
Top