0

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina amesema mawaziri walioteuliwa na Rais John Magufuli si waoga na wanatekeleza wajibu wao ikiwa ni pamoja na kumshauri Rais katika masuala mbalimbali.

Mpina aliyasema hayo jana wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mwandoya wilayani Meatu mkoani Simiyu huku akisikitika kuwa maneno yanayotolewa dhidi ya mawaziri na manaibu na viongozi wa vyama vya upinzani kuwa wao ni waoga na hawamshauri Rais si sahihi.

Alisema baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakibeza utendaji wa Baraza la Mawaziri na kuwaita waoga wasiomshauri Rais.

“Wapo wale wenzetu wa upande wa pili ambao ni wapinzani wamekuwa wakitubeza mawaziri tulioteuliwa na Rais Magufuli kuwa tumekuwa waoga na hivyo kushindwa kumshauri na kulifanya taifa kusinyaa, hii si kweli. Nyinyi ni mashahidi, mmeona jinsi tunavyochapa kazi,” alisema.

Katika kudhihirisha kuwa wanatekeleza wajibu na kumshauri Rais, Mpina alisema Serikali iliamua kumnyang’anya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye shamba la hekta 33 kwa kushindwa kuliendeleza.

“Oktoba 28, mwaka huu, Rais John Magufuli alibatilisha hati ya kumiliki ardhi ya shamba namba 3074 lililopo Mabwepande, Dar es Salaam lililokuwa na hati namba 53086. Jina la mmiliki lililoandikwa katika hati ni Frankline Sumaye huu ni ushauri Rais alipewa na Waziri wa Ardhi na akachukua hatua,” alieleza Mpina.

Alisema wataendelea kuchukua hatua bila ubaguzi wa aina yoyote kwa wasiotaka kufanya kazi kwa kufuata utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Post a Comment

 
Top