0

SEKRETARIETI ya Ajira katika utumishi wa Umma imesema serikali bado imesitisha ajira mpya wakati huu ikiendelea kufanya uhakiki wa watumishi wake pamoja na kupitia upya miundo yake.

Imesema kazi hiyo haijakamilika na kutaka wanaopenda kuajiriwa katika utumishi wa umma kusubiri mpaka pale watakapotangaza kukamilika kwa shughuli ya uhakiki.

Kauli hiyo imetolewa na katibu wa sekretarieti hiyo, Xavier Daudi jana wakati akikanusha taarifa ya tangazo la nafasi za kazi zaidi ya 1,000 serikalini lililosambaa mitandaoni.

“Kama mnavyofahamu serikali ilitoa taarifa ya kusitisha kwa muda ajira mpya serikalini kwa ajili ya kufanya uhakiki wa watumishi wake pamoja na kupitia upya miundo yake, hivyo mpaka sasa mambo hayo yanaendelea na hayajakamilika kwa maana usitishwaji wa ajira bado unaendelea,” alisema.

Katibu huyo aliwataka wadau wote kuvuta subira kipindi hiki wakati uhakiki wa watumishi hewa unapoendelea kufanyika na utakapokamilika na taarifa rasmi ya nafasi wazi za kazi serikalini itatolewa na mamlaka husika hivyo wasikubali kupotoshwa na watu wachache .

Alisema kikundi cha watu kwa makusudi wameamua kusambaza taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii kuanzia Septemba 29 kuwa Sekretarieti ya ajira imetangaza nafasi hizo za kazi zaidi ya 1000, zikiwemo za Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Mtendaji Mkuu wakala wa Misitu Tanzania (TFS ) .

Daudi alisema mtu aliyeanzisha uzushi huo aliingia kwenye tovuti ya Sekretarieti ya ajira na kuchukua matangazo ya Julai 9, mwaka jana, kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili ambayo yalikuwa na jumla ya nafasi 599 na lingine lilikuwa na nafasi za kazi 513.

Aliwataka wananchi kupuuza taarifa kama hizo za uzushi zinapotokea kwani matangazo ambayo hutolewa na Sekretarieti hiyo ni lazima yaonekane kwenye tovuti yake ya www. ajira.go.tz au portal ya ajira ambayo ni portal. ajira.go.tz .

Post a Comment

 
Top