0

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umesema hawamtambui wala hawamtaki katika umoja huo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu wadhifa huo, kisha kuutengua na kurudishwa na msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi.

Aidha wamesema hawategemei kugombana ila wataendelea kuimarisha nguvu ya umoja wao.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe jana alipokuwa akitoa tamko kwa waandishi kuhusu msuguano wa kisiasa unaoendelea hivi sasa ndani ya CUF.

Mbowe alisema kwa kuwa umoja huo unaiheshimu CUF, wanamtambua Julius Mtatiro kama Mwenyekiti na Maalim Seif Sharif Hamad kama Katibu Mkuu, hivyo wataendelea kufanya kazi nao.

Alisema kutokana na mgogoro huo ndani ya CUF, wanawaelekeza wanachama wao, viongozi wa kuchaguliwa na wawakilishi waendelee kushirikiana katika azma ile ile iliyozalisha Ukawa.

Wakati huo huo, mwandishi wetu Lucas Raphael akiandika kutoka Tabora anasema viongozi, wanachama na wapenzi wa Chama cha Wananchi (CUF) mkoani Tabora wamefanya sherehe maalumu kwa kuchinja mbuzi wawili na kula pilau wakipongeza Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi kumrudisha ofisini Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahimu Lipumba.

Katika sherehe hiyo, Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Tabora mjini, Milambo Kamili alitoa tamko rasmi kwa niaba ya viongozi wenzake, wanachama na wapenzi wa chama hicho la kumtambua Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa chama hicho Taifa sambamba na kuwatambua viongozi wote waliosimamishwa akiwemo mbunge wa Jimbo la Kaliua, Magdalena Sakaya.

Post a Comment

 
Top