Kuipitia ukurasa wake wa Facebook Zitto kabwe ameanza kuandika hivi...
Nyerere wangu mimi!
Mwaka 1984 nilianza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kigoma,
katika mji wa Kigoma. Nakumbuka kupelekwa Shule siku ya kwanza na mama yangu
mzazi Bi Shida Salum (Mungu amrehemu) nikiwa sina viatu yaani pekupeku
wala begi la mkononi, nilikuwa nimebeba mfuko wa nailoni. Nakumbuka
usiku wa kuamkia siku ya kwanza kwenda shule, sikulala kwa furaha na
hamu ya kuwa msomi, nilijisikia fahari kuanza shule japokuwa sikuwa na
kitu chochote cha zaida zaidi ya kaptula ya shule na shati liloshonwa
kwa kitambaa cha sanda. Pia nilianza shule nikiwa nimechelewa kwa mwaka
mmoja maana wenzangu walianza wakiwa na miaka 7. Mwaka 1983
nilipopelekwa shule mkono wangu haukuweza kushika sikio upande wa pili,
ambacho kilikuwa kipimo cha kuandikishwa darasa la kwanza.
Hali ya maisha wakati huo ilikuwa mbaya sana. Nakumbuka kwenda shuleni
nikiwa sina kitu tumboni au siku nzima nilikunywa uji usio na sukari.
Uji wenyewe ulikuwa ni wa unga wa njano uliotokana na mahindi ya njano
ambayo tuliambiwa nchi yetu ililetewa kama msaada kutoka nchini
marekani.
Shule yetu kama zilivyokuwa shule
nyingi za wakati huo hatukuwa na madawati ya kutosha na vyumba vya
madarasa vilikuwa vichache sana. Ilikuwa ni kawaida kwa wadogo (darasa
la kwanza mpaka la tatu) kusomea chini ya mwembe na kukaa juu ya
matofali. Hali hiyo ilipelekea kaptura yangu ya shule kuwekwa viraka
vingi maana ilikuwa inachanika mara kwa mara. Nyakati nyingine ilibidi
kwenda shuleni na shati likiwa halijakauka hasa siku za alhamis, siku ya
usafi na iwapo nikiwa zamu ya mchana kwani nilikuwa nina shati moja tu
tena lililotokana na kitambaa cha sanda.
Kwa dhahiri, watoto wa masikini na
matajiri tulikuwa shule moja, darasa moja hata wote kukaa kwenye
matofali. Watoto watawala na watawaliwa tulicheza mpira pamoja, kuruka
dana na hata kuruka kamba. Hatukujisikia wanyonge kwa sababu hatuna
viatu au kuvaa kaptura zenye viraka na mashati ya sanda. Kamwe sikumbuki
kudharauliwa shuleni sababu ya uduni wa maisha yangu. Heshima ilitokana
na uwezo wako darasani na kupitia hilo nilipata marafiki wa kutoka
madaraja yote ya maisha. Nakumbuka mtoto wa Mkurugenzi wa Maendeleo Mkoa
wa Kigoma ndugu Daniel Masanja ndiye alikuwa rafiki yangu wa karibu na
kwa kuwa sikuwa na hata pesa ya kununua bajia wakati wa mapumziko, yeye
alikuwa ananinunulia.
Huko baadaye, ada yangu ya kidato
cha kwanza ililipwa na Mzee Sebastian Kasomi ambaye mwanaye Kasomi
Mabula alikuwa rafiki yangu mkubwa mara alipohamia shuleni kwetu
akitokea mjini Shinyanga. Mzee Kasomi alikuwa Mkuu wa idara ya Kodi ya
Mapato mkoani Kigoma.
Licha ya uduni wa maisha watoto
wengi tuliishi kwa matumaini makubwa sana. Mwalimu wetu Mkuu ndg. Daniel
Andulile alikuwa mkali sana kwa watoto wote bila kujali daraja la
maisha la wazazi wao. Alikuwa anatucharaza viboko kwa makosa na utundu
bila ubaguzi. Alisisitiza sana kusoma kwa bidii ili kujenga Taifa. Dhana
hii ya kujenga Taifa iliingizwa kwenye akili zetu na sisi kumeza bila
kujali maana yake. Wakati mwingine tulikuwa tunarudi nyumbani huku
tukijadili kitoto kuwa tunajenga Taifa. Kila siku mwendo wa kilometa
Sita kwenda na kurudi shuleni.
Elimu hii isiyo ya kibaguzi sasa
najua ilitokana na sera za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere. Jitihada zangu darasani ndio ziilikuwa kipimo cha utu wangu na
sio uwezo wa kiuchumi wa wazazi wangu.. Elimu iliyompa fursa sawa za
kuendelea na kusonga mbele mtoto aliyekuwa kigoma, kantalamba au Dar es
salaam. Elimu iliyokuza ndoto, kuinua ari na kujenga matumaini ya kila
mtoto wa kitanzania. Elimu iliyovunja na kusambaratisha matabaka ya
kiuchumi na dhamana. Elimu iliyojenga uzalendo na hamasa ya kutumikia
taifa letu kwa misingi ya haki, uadilifu na upendo.
Sikuwahi kukutana na Mwalimu Nyerere
isipokuwa niliwahi kumwona akiwa ndani ya gari nikiwa nimepanga mstari
barabarani alipofanya ziara mkoani kwetu mwaka 1987 nikiwa darasa la
nne. Lakini nilikuwa kama ninaishi naye kutokana na namna nilivyotaka
kuwa kama yeye. Nikiwa darasa la pili nakumbuka katika mkebe wangu (
mathematical set) mkuu kuu niliweka picha ya kukatwa kutoka kwenye
gazeti ya Mwalimu na Kawawa. Na nilijisikia fahari kuwa na picha zao,
mara zote nilipokuwa nafungua mkebe kutoa kalamu nilijisemea kimoyomoyo,
“siku moja nitakuwa kama wewe”
Licha ya maisha magumu tuliyokuwa
tunaishi, maisha ya kupanga mawe kwenye mstari wa kununua mahitaji
muhimu kama sukari, sabuni na mafuta kutoka duka la ushirika, maisha ya
kushindia uji wa yanga na kutembea mwendo mrefu kwenda shuleni, niliishi
kwa imani kubwa kuwa mimi na watoto wengine tupo sawa. Usawa katika
kupata elimu, usawa katika kucheza na usawa katika ndoto na matumaini.
Nimemaliza elimu ya Chuo Kikuu, ndoto niliyoruhusiwa kuwa nayo kwa
sababu ya sera za Ujamaa, za Mwalimu Nyerere.
Ujamaa haukuwa katika usawa wa elimu
tu ambapo kila mtoto alipata elimu bure na bora katika Shule za umma
bila ubaguzi bali pia namna jamii iliishi. Mtoto alikuwa analelewa na
jamii nzima. Ukifanya makosa mtaani mzazi yeyote anakuadhibu ili
kukurekebisha. Ukifanya jambo jema, mzazi yeyote anakupongeza.
Mwaka 1985 mwezi Novemba nilipokuwa
natoka shuleni, karibia na Benki ya Taifa ya Biashara Tawi la Obed
Katikaza, nilikutana na Mama Colleta Furugunya tuliyekuwa tunaishi mtaa
mmoja na nikimwita bibi Colleta. Aliponiuliza matokeo yangu ya mtihani
wa kumaliza muhula wa pili wa darasa la pili kwa kujiamini nikampa
karatasi yangu ya matokeo. Nilikuwa nimeshika nafasi ya tatu darasani
nyuma ya Ramadhan Kalukula na Haki Manyaga. Bibi Colleta alinishika
mkono mpaka duka la Viatu, Bora Shoes na kuninunulia jozi yangu ya
kwanza ya viatu. Viatu vile viliitwa Asante Salim, aliyekuwa Waziri Mkuu
wa mwisho wa Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa anajaribu kubadili hali
mbaya iliyokuwepo. Hivyo ndivyo nilivyopata viatu vyangu vya kwanza vya
shule. Shukrani kwa sera nzuri ya ujamaa, mshikamano na upendo.
Hizo ni enzi.
Post a Comment