0

Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya jana alikaliwa kooni na mawakili wa wadai katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi 2015 wakimtaka kutoa ufafanuzi wa idadi ya wapigakura waliojiandikisha kwenye daftari la wapiga kura.


Katika uchaguzi mkuu wa ubunge Jimbo la Bunda Oktoba 25, 2015, Bulaya alimbwaga mgombea wa CCM na mwanasiasa mkongwe, Stephen Wasira lakini wapigakura wanne walifungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kupinga matokeo. Ester alikuwa mbunge wa viti maalumu CCM, lakini alihamia Chadema na kumshinda mkongwe Wasira.


Katika kesi hiyo ambayo vikao vyake vinafanyika mjini Musoma na ikiwa ni siku yake ya kwanza kutetea ubunge wake, Bulaya alibanwa na mawakili wa walalamikaji wanaopinga ushindi wake baada ya idadi ya wapiga kura iliyoandikwa kwenye kiapo chake kuwa tofauti na iliyoandikwa na msimamizi wa uchaguzi kwenye fomu namba 24B ya matokeo ya uchaguzi.


Bulaya alidai idadi ya wapiga kura walioandikishwa katika fomu ya matokeo namba 24B aliyopewa ilikuwa 69,369 lakini imetofautiana na aliyokuwa nayo msimamizi wa uchaguzi ambayo kuna jumla ya wapiga kura 69,460 baada ya kujumlisha kura zote.


Wakili wa upande wa mleta maombi, Hajra Mungula alitaka kujua kutoka kwa mbunge huyo idadi ipi sahihi kati ya ile aliyoandikiwa na msimamizi wa uchaguzi kwa mkono baada ya kuikataa ile ya kwanza na kutangaza idadi ya wapigakura wa wilaya nzima ya Bunda ambao ni 164,794 au ile iliyotangazwa na msimamizi huyo.


Mbunge huyo alidai kuwa wakati msimamizi anabadilisha idadi hiyo hakuona takwimu sahihi wakati anaandika kwa kuwa alikuwa amekaa mbali kidogo ila aliamini kilichokuwa kinaandikwa na msimamizi huyo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Lucy Msofe


Wakili huyo alitaka kujua ilikuwaje hadi akaijua idadi hiyo ya wapiga kura wa wilaya nzima waliojiandikisha ambao ni 164,794 wakati hajui idadi ya wapigakura katika majimbo mengine ya wilaya hiyo? Mbunge huyo alijibu kuwa yeye aliifahamu idadi hiyo baada ya kupitia daftari la wapiga kura kabla ya uchaguzi kuanza.


Alidai alifahamu idadi hiyo kwa kuwa aliwahi kuwa diwani na alishakuwa kiongozi kabla ya kuwa mbunge na kusema kuwa taarifa za idadi ya wapiga kura kwa kawaida siyo siri.


Mbunge huyo alieleza kuwa tofauti ya idadi ya wapiga kura 69,460 na 69,469 haikuwa sawa lakini pia haikuathiri matokeo ya uchaguzi katika jimbo hilo wala kuathiri idadi yoyote ya wapiga kura kwa kuwa tofauti hiyo ni ndogo sana.


Alipohojiwa na wakili wa mleta maombi wa tatu Constantine Mutalemwa, “Ni nani aliyeziingiza takwimu hizo zinazopishana kwenye fomu namba 24B ya matokeo ya uchaguzi, Mbunge huyo alijibu kuwa aliyeingiza takwimu hizo kwenye fomu namba 24B ni msimamizi wa uchaguzi.


Mawakili wa upande wa Serikali ni Angela Lushagala na Michael Haule; Bulaya anatetewa na Tundu Lissu huku upande wa waleta maombi watatu mawakili ni Yasini Membe, Hajra Mwingula na Constantine Mutalemwa.


Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa katika mahakama hiyo chini ya Jaji Noel Chocha.

Post a Comment

 
Top