SERIKALI
imewaondoa watumishi hewa 17,201 katika utumishi wa umma, ambapo licha
ya kupokea mishahara pia mikopo mingi ilitolewa visivyo.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Angella Kairuki alisema hayo jana mjini Dodoma wakati wa kuapishwa
kwa wakurugenzi watendaji wapya 13 walioteuliwa Septemba 10, mwaka huu
na Rais John Magufuli.
Kairuki
alisema kuanzia Machi mwaka huu hadi sasa wameondoa watumishi hewa
17,201 kwenye utumishi wa umma na zoezi hilo bado linaendelea.
“Tumegundua mikopo mingi imetolewa visivyo,” alisema Kairuki na kuongeza kuwa asilimia 80 hadi 90 ya watumishi hewa ni watoro.
“Kwenye
sekta ya elimu kuna Mratibu wa elimu kata, maofisa elimu lakini
wamekuwa hawafuatilii walimu wengi wamekuwa hawapo kwenye vituo vya kazi
lakini wanapokea mishahara,” aliongeza waziri huyo na kubainisha kwamba
kumekuwa na tabia ya walimu ambao hawako kazini kwa kipindi kirefu,
lakini walimu wenzao wamekuwa wakiwaandikia kwenye kitabu cha mahudhurio
na kuwasainia ili kuonesha kuwa wapo kazini, jambo ambalo ni kinyume
cha utaratibu.
“Mwarobaini
wa walimu wanaowajazia vitabu vya mahudhurio walimu ambao hawafiki
kazini dawa yao iko jikoni, tutafuatilia kituo kimoja hadi kingine
kuwabaini na tutachukua hatua,” alieleza na kuongeza kuwa maofisa
utumishi wengi wamekuwa wakijifanya ndio wakurugenzi jambo ambalo
limekuwa likisababisha tatizo la watumishi hewa kuendelea.
Alisema
michakato ya maombi ya watumishi inaanza Novemba, hivyo wakurugenzi
wahakikishe wanaletewa ikama wajiridhishe ili wapate watumishi kulingana
na mahitaji. Akizungumzia suala la watumishi hewa, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene
alisema “Hatuwezi kuajiri wakati tuna hewa lazima tuchambue na
kujiridhisha.”
Pia
alisema mitandao ya kijamii ni janga kubwa kwani kuna watu wanatoa
taarifa mitandaoni kuwa ni taarifa ya waziri kumbe uongo. “Utakuta mtu
kakataa kaandika speech ya Waziri, kila mtu anayeweza anachapisha, wapi
nilisema walimu wa sanaa hawataajiriwa?” Alihoji.
Alisema
hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii watu waliweka taarifa kuwa
Tamisemi inaajiri na watu watume maombi jambo ambalo lilileta usumbufu
mkubwa.
Aidha,
alisema watu wanahoji uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga aliyekuwa mtangazaji wa Clouds Tv, lakini
ukweli ni kuwa aliteuliwa kulingana na sifa na uwezo.
Rais
ana mamlaka ya kuteua mtu yeyote ambaye anaamini anaweza kufanya kazi,
Wizara hii iko chini ya Rais,” alisema na kuwashangaa watu wanaobeza
uteuzi huo na kutaka wakurugenzi hao wakachape kazi.
|
Post a Comment