Neno “Ukuta” limekuwa ni neno maarufu kwa sasa nchini Tanzania
kutokana na namna lilivyotumiwa na Chama cha upinzani cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) karibu mwezi mzima sasa kama sehemu ya kudai haki
yao kwa serikali ya Tanzania kwa yale wanayoyaona hayapendezi kwao
kulingana na wao binafsi wanavyosema na kudai zaidi na si mimi. Chama
cha chadema kimejipanga kufanya maandamano ya kudai haki hiyo siku ya
tarehe mosi mwezi ujao wa tisa ambayo itakuwa ni siku ya alhamisi,
ingawa serikali imeshapinga kutokufanyika kwa maandamano hayo na kuonya
watu wasijaribu kufanya hivyo kwani kwa kufanya hivyo itakuwa ni kosa
kisheria kutokana na kutokufuata sheria na marufuku hiyo iliyotolewa na
serikali kuhusu maandamano hayo.
Mbali na hayo mimi si mwanasiasa na makala hii haipo kwa ajili ya
kuzungumzia masuala ya siasa au kutoa taarifa yoyote ile kwa lengo la
uchochezi wa masuala ya siasa au masuala yoyote yale yanayohusiana na
suala hili la ukuta, bali makala hii nimeitoa kwa ajili ya kijikita
zaidi katika kukuhamasisha wewe msomaji wangu binafsi hasa kwa ajili ya
kuchukua hatua juu ya maisha yako kwa lengo la kujiletea maendeleo
binafsi kwako. Nimetumia neno “ukuta” ambalo linatumiwa na chama cha
chadema kwa ajili kuhamasisha wafuasi wao kuandamana na kudai haki kwa
serikali na zaidi likiwa na maana ya “kuiwekea ukuta serikali kwa yale
ambayo chadema inaona inaonewa kwa sasa wao na wananchi wote.”
Kwa mfano utakumbuka masuala ya Ukuta wa Berlin (kijerumani Berliner Mauer)
ulitenganisha sehemu mbili za jiji la Berlin (Ujerumani) kuanzia 13
Agosti 1961 hadi 9 Novemba 1989. Mashariki ya Berlin ilikuwa sehemu ya
nchi ya kikomunisti Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani na magharibi ya
jiji ilikuwa chini ya mamlaka ya Marekani, Uingereza na Ufaransa. Ukuta
huu ulikuwa na urefu wa kilomita 45.3 ukiwa sehemu ya mpaka kati ya
madola mawili ya Ujerumani yaliyokuwepo kuanzia 1949 hadi 1990. Ukuta wa
Berlin ulikuwa mfano uliojulikana zaidi wa “pazia la chuma” katika
Ulaya lililotenganisha nchi za kikomunisti za Ulaya mashariki na nchi za
Ulaya magharibi. Takriban watu 200 waliuawa walipojaribu kuvuka ukuta
kutoka mashariki kwenda magharibi.
Chanzo cha ukuta huu ulikuwa ugawaji wa jiji la Berlin baada ya Vita
Kuu ya Pili ya Dunia tangu 1945. Nchi washindi ziliamua kugawa Ujerumani
yote wakaanzisha kanda nne zilizotawaliwa na Umoja wa Kisovyeti,
Marekani, Uingereza na Ufaransa. Berlin ilikuwa ndani ya kanda ya
kisoyeti lakini ikiwa mji mkuu wa Ujerumani ilitangazwa kuwa mkoa wa
pekee ikagawiwa pia katika kanda nne za washindi. Tangu 1946 washindi
walianza kutoelewana na kipindi cha vita baridi kilianza ambako nchi za
magharibi (Marekani, Uingereza, Ufaransa) zilisimama dhidi ya nchi za
mashariki zilizoongozwa na Umoja wa Kisovyeti. Ukifatilia suala hili la
ukuta kwa israel na palestina utakuna nalo pia.
Tukiachana na mfano huo basi tambua Neno ukuta linajulikana maana
yake na kwa maana yake ya kawaida tu ni kwamba, “ukuta ni kizuizi
kinachojengwa kwenye nyumba au jengo kwa ajili ya kuziba uwazi unaoweza
kujitokeza katika nyumba au kuikamilisha nyumba au jengo hilo kuwa
kamili.” Ndio maana waswahili wa kale walisema, “usipoziba ufa (uwazi
uliojitokeza), utajenga ukuta (yaani utang’aramia kujenga ukuta mkubwa
zaidi au ukuta mzima ili kuziba sehemu kubwa zaidi ya uwazi
uliojitokeza).
Pamoja na maana hiyo ya kawaida kabisa ambayo tumeipata au
nimekupatia hata kabla ya kuingia kwenye kamusi ya kiswahili sanifu
kuitizama na kuangalia maana yake kamili ya neno hilo hasa kwa kuwa ni
neno jepesi kueleweka kwa kila mtu. Wapo watu wamekuja na maana nyingine
nyingi ya neno hili “ukuta” kutokana na kuwa maarufu zaidi hasa katika
kipindi hiki ambacho Chama cha Chadema wamelipa “promo” kubwa neno hilo,
na kuenea nchini kote hadi kwa watoto wadogo na wao wakiwa wanajua nchi
yetu ya Tanzania kwa sasa habari ya mjini ni neno “ukuta”.
Kuna watu wametoa maana kadhaa ya neno “Ukuta” sitoweza kuzitoa
mahali hapa kutokana na sababu maalum na yawezekana nawe umeshakutana
nazo huko mtaani kwako au kwenye mitandao ya kijamii. Ila leo hii nataka
utumie neno hili na maana yake ya kwanza hasa niliyokupa hapo juu kama
sehemu ya kukusaidia wewe binafsi katika kufikia mafanikio makubwa hasa
juu ya ndoto na malengo yako. Yapo maeneo unayohitaji kuweka ukuta
katika maisha yako binafsi ili uweze kufanikiwa katika viwango vya juu
na kufikia katika hatua ya kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
Ili ufanikiwe ni lazima ufikie mahali ambapo utaweza kukabilina na
mambo yanayokuzia kuendelea mbele wewe mwenyewe binafsi au wakati
mwingine kuyakingia “ukuta” ili yaweze kuzuilika na wewe uweze kuendelea
mbele zaidi. Kama kujenga ukuta ni sehemu ya kuziba nyufa au matundu au
uwazi unaojitokeza kwenye nyumba au jengo lako, basi hata mtu binafsi
anaweza kujenga “ukuta” kwa ajili ya maeneo yaliyojitokeza kwenye maisha
yake na kuweka uwazi au nyufa au matundu yanayoweza kuwa sababu ya mtu
huyo kutokuendelea mbele. Jiulize una ufa au uwazi au tundu gani katika
maisha yako lililojitokeza na linaloruhusu kukwama kwako na kukuzuia
kuendelea mbele zaidi? Na kumbuka “usipoziba ufa, utajenga ukuta mkubwa
zaidi, na wakati mwingine watu watakuchungulia au utawapa nafasi wezi
kuingia ndani kwa haraka na kukuibia kila kitu.”
Unahitaji kuziba ufa (nafasi ndogo au kubwa) na kujenga ukuta katika
maeneo yafuatayo ndani ya maisha yako ili uweze kusogea mbele na
kusababisha mafanikio yatokee katika maisha yako.
1: Ziba ufa au milango ya hofu uliyonayo na jenga ukuta wa kujiamini ili usogee mbele kimaisha.
Hofu ni ufa, hofu ni uwazi, hofu ni tundu linaloweza kusababisha
mafanikio yako yasitokea hasa kwa watu wengi walio na ndoto ya kufikia
ndoto zao kubwa walizonazo katika maisha. Angalia ni mambo mangapi
umeacha kuyafanya kwa sababu ya hofu ya kuogopa kufeli au kushindwa
njiani, angali ni mara ngapi umepata mawazo mazuri ya kukusogeza mbele
kimaendeleo laini umekuwa na tabia ya kughairisha kuyatekeleza hadi
yakapotea nadni ya moyo na akili yako. Tambua hofu ni mlango husio mzuri
unaohitaji kuuziba kwa ukuta ili uweze kujenga mlango wa kujiamini na
kuweza kuruhusu tabia njema kuingia ndani yako na wewe kusogea mbele.
Unahitaji kujenga ukuta wa kujiamini kwenye maisha yako ili uweze
kuona matunda unayotaka kuyaona kwa kipindi kirefu cha maisha yako
ulichoishi hapa duniani. usikubali kuishi chini ya kiwango cha maana
halisi ambayo Mungu amekupangia uishi bali amua kupigania ndoto yako
usiku na mchana hadi uhakikishe unaona matokeo chanya maishani mwako.
Soma makala ya Aina 5 za hofu unazotakiwa kuzikabili ili kujiletea ushindi katika ndoto yako.
2: Ziba ufa au mlango wa kujitetea na kuacha kutekeleza
wajibu wako na jenga ukuta wa kuchukua hatua kivitendo zaidi ili kufikia
ndoto yako.
Wapo watu wengi kiukweli ni wazuri sana katika kuongelea habari nzuri
za mafanikio au watu waliofanikiwa na wengine hata kuziandika vizuri
kama ninavyoandika mimi mahali hapa kila siku, lakini watu hawa si watu
wenye kuchukua hatua kivitendo na kuwa watu wenye kutekeleza wajibu wao
walionao kwa ajili ya kufuata ndoto zao za Maisha walizonazo ili kuleta
matokeo makubwa katika maisha yao.
Kujitetea ndio jambo kubwa linalojitokeza kwa watu hawa, kwani kila
unapojaribu kuwaambia wanaweza kufanya jambo fulani na kufanikiwa
watakupa sababu lukuki zinazoweza kutumika kama ufa au mlango au tundu
la kuwazuia wao kusogea mbele na kufikia hatua ya juu ya mafanikio yao
wanayoyataka. Unakutana na mtu anayehitaji kufanikiwa kiuchumi na kuwa
na uhuru wa kifedha lakini unapomshirikisha juu ya habari ya kuweka
akiba zaidi ama kuwekeza anakupa sababu ya kutoweza kufanya hivyo kwa
kuwa hana kipato cha kutosha; mwingine unapomshirikisha habari ya kuanza
biashara hata ndogo ndogo akiwa bado ameajiriwa (part time business)
anakuambia siwezi kwa kuwa mambo ya ofisini yamembana lakini mtu huyu
anataka kuwa milionea na mtu mwenye mafanikio kifedha. Nakuambia kweli
sahau kuhusu mafanikio kama wewe ni mtetezi wa hali mbaya inayokukabili
maishani mwako.
“Huwezi kufanikiwa kwa kujitetea, bali waliofanikiwa waliamua kuondoa hofu wakajiamini na kuchukua hatua kivitendo.” – Wilfred Tarimo (me)
3: Ziba ufa au mlango unaopitisha tabia ya ubinafsi ndani yako na jenga ukuta wa kushirikiana na wenzako katika maendeleo.
Kuna watu wana tabia ambazo zimekuwa ni chachu mbaya kwao ya kuwazuia
kusogea mbele katika mafanikio makubwa kimaisha. Tabia kama vile ya
kutojitoa kikamilifu katika kitu anachokifanya ili kuleta matokeo
makubwa, uvivu na kuendeleza usingizi husio na faida juu yake, chuki na
ubinafsi, nakadhalika. Yote hayo na mengine mengi yamefanyika kuwa
mlango na ufa mkubwa katika maisha ya watu wengi na kuwazuia kuendelea
mbele na kufikia katika hatima njema ya ndoto zao. Usipoziba ufa huu,
utajenga ukuta mkubwa zaidi hapo badae.
Tabia ya ubinafsi ndio imekuwa chachu mbaya kwa wengi kutokufanikiwa.
Kuna wakati nilipoanza kuwa mwandikaji na mchapaji wa makala mtandaoni
kama ninavyoendelea kufanya hivi sasa tangu 2012, watu wengine wenye
mitandao kama mimi ya uandishi wa makala wakaibuka na kusema nachukua
makala zao na kuandika. Nilishangaa sana huku mimi mwenyewe binafsi
ninajua namna ninavyoumiza kichwa usiku na mchana ili kujua ninaandika
nini cha kuweza kuwasaidia watu kufikia ndoto zao. Ninajua
ninachokiandika kwa kuwa ninayoyandika kuna mengine nimeyapitia na
kuyafanya kivitendo hata kuzaa matokeo chanya kwangu kwani siwezi
kuandika kitu ambacho mimi binafsi sikitekelezi au sijaona bado matokeo
yake, ila mengine ninajifunza kila siku kwa kusoma vitabu mbali mbali
vya watu waliofanikiwa.
Jiulize inakuaje mtu anatokea anasema unaandika mambo ninayoandika
mimi, kama ni hivyo basi haina haja ya kuwa na waandishi wengi duniani
ila ni wewe tu uliye mwandishi au haina haja ya kuwa na waimbaji wengine
ila ni wewe tu uliyeitwa kuimba. Si kweli kwamba ni mtu pekee tu mmoja
ndiye aliyeitwa kuandika au kuitwa kuimba peke yake, ila ni ubinafsi na
hofu ya kupitwa na mwingine anayemwona anampa changamoto juu yake ndio
maana anampinga badala ya kujifunza kutoka kwake na kutumia njia hiyo
kama changamoto ya kumfanya kuwa bora zaidi. Kama unasoma kitabu kile
kile cha Robert Kiyosaki ukaelezea au kuwafunza watu, na akaja mwingine
kuandika kwa utaalamu zaidi yako, wewe unaumia nini. Huo ni ubinafsi, na
hii ndio sababu ninayokupa kwa nini watu wengi hawatoweza kufikia
mafanikio makubwa wanayoyataka au kuyasema ni kwa sababu ya ubinafsi
walionao ndani yao. Na kama ndio hivi nchi ya Marekani isingetoa
waandishi wengi waliondika vitabu vyao binafsi tunavyovisoma hivi leo.
Ondoa ubinafsi ndani yako na jenga ukuta wa kuuzuia usirudi kwa upya
ndani yako ili ufanyike kuwa mfano wa kuigwa na wengi na hatimaye uweze
kujiletea mafanikio makubwa katika maisha yako. Nakushauri ungana na
watu waliofanikiwa na kuwa miongoni mwa washindi walioamua kujitoa kwa
ajili ya kuhakikisha wanageuza maisha yao kuwa katika muonekano mpya
zaidi kila siku. Usikubali kwenda peke yako, karibu ujiunge na kundi la
whatsapp la “ishi ndoto yako” ili uweze kufikia ndoto yako pamoja na
wengine. Tuma jina lako kamili na namba yako kwa kupitia namba ya simu
iliyopo hapo chini ili kujiunga na kundi hilo na zaidi utaweza kujifunza
mambo mengi zaidi ndani ya kundi hilo yatakayokupa hatua mpya kila
siku.
Karibu ujiunge na hawa watu wa “umoja wa kupinga umasikini tanzania
(ukuta)” ili uweze kujifunza mambo ya kukupeleka katika hatima njema ya
ndoto yako. Kubali kuziba ufa, ili husije kujenga ukuta mkubwa zaidi
maishani mwako. Jenga ukuta katika mambo yote yanayokuzia kuendelea
mbele katika maisha yako, ili uweze kusogea mbele kimaendeleo wewe
mwenyewe binafsi kabla ya kwenda mbele kama nchi au taifa kiujumla, bali
anza na wewe kwanza.
JIAMINI NA AMINI UNAWEZA. ISHI NDOTO YAKO.
Post a Comment