Tunapoongelea suala hili au neno mafanikio, kila mtu huwa ana maana
yake kulingana na maana yake anayokuwa nayo kwa wakati wake na kwa eneo
lake husika analohitaji mafanikio hayo yatokee katika maisha pia
kulingana na ndoto yake aliyonayo. Nikiwa na maana kuwa kila mtu ana
tafsiri yake kuhusu mafanikio kutokana na muda na wakati alionao na
anaoendelea kuuishi hapa duniani. Kwani kuna Mafanikio mengi kutokana na
mtu mwenyewe binafsi kwa muda wake husika anaohitaji mafanikio hayo na
kwa njia hiyo ndio maana huleta tafsiri halisi ya yeye kuelewa kile
anachotaka kufanikiwa kwa wakati huo aliokuwa nao.
Kuna mafanikio ya kiafya, kuna mafanikio ya kiuchumi na kifedha na
kuna mafanikio ya uhusiano mzuri nakadhalika Yote hayo na mengine mengi
ni sehemu mojawapo ya maeneo ambayo kila mtu anahitaji kufanikiwa
kutokana na kipindi na muda husika alionao duniani.
Katika makala yetu hii nitazungumzia zaidi juu ya mafanikio ya
kiuchumi na kifedha, hasa kwa mtu binafsi anayehitaji kuishi akiwa na
uhuru wa kifedha na uchumi katika maisha yake hapa duniani.
Zipo siri nyingi ninazoweza kukupa na zikakusaidia kufanikiwa katika
eneo hili la uchumi na fedha, lakini ndani ya makala yetu nitazungumzia
juu ya siri saba muhimu ambazo ndio ngunzo kuu ya kukusaidia kufikia
mafanikio makubwa ya kiuchumi na kifedha, na hata katika maeneo mengine
ya maisha yako kama vile afya, mahusiano nakadhalika hutumika.
Hivyo ni muhimu kuishi maisha ya mafanikio iwe katika suala la uchumi
na fedha, uhusiano, imani na afya. Kwa kuzingatia jambo hilo ni muhimu
uzingatie kanuni na siri zifuatazo:
Siri ya Kwanza:
Tembea katika Imani sahihi na Ibada.
Katika jambo lililo la muhimu na kipekee ambalo mtu yoyote
anayehitaji kufanikiwa katika maisha yake anapaswa kulifanya ni kuishi
maisha ya imani na kuwa mtumwa wa ibada iliyo sahihi. Fahamu katika
mambo yote saba nitakayozungumzia hapa suala la imani na ibada ni la
muhimu sana na ni vyema niseme linafaa kuwa la lazima kufanywa kila mara
na mtu anayehitaji mafanikio makubwa maishani mwake.
Hakuna njia ya kufanikiwa na yenye mafanikio ya kudumu katika maisha
haya pasipo kuwa na uhusiano wa imani uliyonayo. Ndio maana wapo watu
wanaoenda kwa waganga wa kienyeji kwa ajili ya kupata mali na utajiri
wanaohitaji, na wapo wanaomwamini Mwenyezi Mungu kama ndiye msaada wao
katika maisha ya kufanikiwa kwao. Ninakataa nji ya kwenda kwa waganga wa
kienyeji kwani sio njia nzuri unayotakiwa kuifuata bali kubali
kumwamini Mwenyezi Mungu pekee kama chanzo cha kufanikiwa kwako.
Narudia tena ya kwamba; yote kwa yote katika hayo sawa na unavyoamini
wewe binafsi la muhimu kwangu kukufahamisha katika hili ni kwamba; ni
vyema uwe na imani na ibada katika kile unachokiamini ili uweze kupata
baraka na mafanikio ya kweli maishani mwako. Lakini nakupa ushauri ni
vizuri hasa Umwamini Mwenyezi Mungu zaidi ya vitu vingine vya kupita.
Jifunze kuwa na ibada kila mara na tambua binadamu si kazi ya mikono
yetu binafsi, bali ni kazi iliyotokana na Mungu mwenyezi mwenyewe na
kila mwanadamu ana fungu lake jema mbele ya Mwenyezi Mungu aliyemuumba.
Usimkimbie Mungu ukatafuta mambo mengine yasiyofaa huku yeye ndie chanzo
cha wewe kuwepo hapa duniani na anafahamu njia zako zote za kupata
mafanikio.
Siri ya Pili:
Kufanya Kazi kwa bidii na ufanisi.
Suala nzima la kufanikiwa katika maisha linahitaji kujitoa na
kujikana kila mara iitwapo leo ili kuhakikisha unafanikiwa na kuwa na
mwelekeo mzuri na mwema wa kimaisha. Kufanya kazi kwa bidii huendana na
ufanisi na ujuzi wako ulionao ambao katika vyote hivyo kwa pamoja
ukizingatia vitaleta matokeo chanya na makubwa katika maisha yako na
hatimaye kufanikiwa.
Acha kuwa mtu wa malalamiko na kukata tamaa kwa haraka, bali anza
kuanzia sasa kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza kipato
chako cha kila siku unachohitaji kuwa nacho. Utajiri hautokei kwa gahfla
tu kama wengi wetu tunavyozani bali kama unahitaji kufanikiwa kifedha
na kiuchumi ni muhimu ujitoe kufanya kazi halali na tena kwa kujituma na
kwa ufanisi mkubwa.
Siri ya Tatu:
Kutoa nafasi ya Kujifunza zaidi.
Kusoma mambo mbali mbali yahusuyo maisha na yanayohusu kile kitu
ulichowekeza maishani mwako kukifanya; hiyo ni sehemu tosha inayoweza
kukubadilisha fikra zako na kukufanya kuwa bora, mtaalamu na mfanisi
mkubwa katika utafutaji wa mafanikio yako. Hivyo basi unahitaji kuwa
msomaji zaidi wa masuala mbali mbali yanayogusa eneo la maisha yako,
mafanikio yako na uchumi wako kiujumla; ili kukupa ujuzi na utaalamu
mkubwa wa namna ya kufanya.
Tambua ninapozungumzia suala la kusoma sina maana ya kwamba unatakiwa
uingie darasani tu, HAPANA. Hapa nina maana kwamba ujifunze kusoma
mambo hata yale ya kawaida kabisa yahusuyo maisha ya mafanikio yako
binafsi zaidi. Kama vile ulivyotoa muda wako kwa wakati huu kusoma
makala hii katika mtandao huu, hakikisha tabia hii uliyoianza isiondoke
kwako kabisa bali uiendeleze kwa bidii na juhudi kubwa kila siku
maishani mwako.
Nakusihi anzisha tabia ya kusoma vitabu mbali mbali vinavyohusu au
kuzungumzia masuala ya maendeleo ya mtu binafsi, utajiri, kuwekeza, afya
na usafi, ufanisi wa kazi, masoko, nakadhalika. Vitabu kama vile Self
Made Millionare, Rich Dad Poor Dad, Maximum Achievement, The power of
positive thinking, Think Big By Donald Trump, Hisa, Akiba na Uwekezaji,
nakadhalika.
Tembelea mitandao mbali mbali yenye kutoa elimu na mafunzo mbali
mbali ya kibiashara, maendeleo ya mtu binafsi, utajiri na kuwekeza,
nakadhalika. Mitandao kama vile huu wa CICBAT na mingine mingi iliyopo kwa sasa utajifunza mambo mengi ya kukusaidia kutimiza ndoto yako.
Siri ya Nne:
Kuwa na Uhusiano Mzuri na watu waliokuzunguka au unaokutana nao kila siku.
Katika dunia ya leo kama unahitaji kufikia mafanikio makubwa zaidi
maishani mwako hili ndio jambo au siri na la muhimu zaidi unalopaswa
kulitekeleza kwa haraka kwa kuzingatia umakini mkubwa wa kufanya hivyo.
Unahitaji watu makini na wenye moyo wa utayari wa kuweza kukusaidia ili
uweze kufikia katika hatua ya mafanikio yako makubwa.
Kuwa na uhusiano mzuri na watu wa karibu yako ulionao ni jambo jema
linaloweza kukuweka katika mazingira mazuri zaidi ya mafanikio makubwa
na ukawa mtu wa tofauti na wengine katika nyanja zote za kimaisha. Kama
ukikosa uhusiano mzuri na watu kuna athari kubwa ya kukosa furaha na
amani; na kama ukikosa furaha na amani kuna athari kubwa pia ya kukosa
uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi na bidii, kwa sababu umekosa furaha
inayokufanya uwe mwenye amani wakati wote katika mazingira ya kazi na
watu wengine kiujumla.
Siri ya Tano:
Kuwa na Nidhamu ya Kutunza Muda ulionao.
Hili ni jambo ambalo watu wengi wa jamii yetu tuliyonayo wameshindwa
kulifanikisha kwa asilimia kubwa katika mazingira yao yote ya kimaisha
na kazi, hivyo limesababisha watu wengi kushindwa kufikia malengo
makubwa na mazuri waliojiwekea maishani mwao. Nataka nikuambie muda ndio
msingi mkubwa na wa kipekee wa kukusaidia kufikia katika malengo yako
yote uliojiwekea na unayotaka yafanikiwe kwa ajili ya kutimiza ndoto
yako na kufikia mafanikio ya kweli unayoyahitaji.
Huwezi kufikia mafanikio makubwa na kufanikisha malengo yako kama
bado hauna nidhamu ya kutosha ya kutunza muda ulionao kila siku. Kila
mwanadamu anayeishi chini ya jua amepewa masaa 24 ya kufanya kazi na
kufanya mambo mengineyo, na kwa kupitia masaa haya 24 ndio utakapoamua
unahitaji kufanikiwa au kutokufanikiwa kwa kiwango gani kila siku ili
kufikia malengo yako.
Jifunze kwenda na muda ili uongeze ubora wako, heshima yako na
nidhamu yako binafsi katika maisha yako na eneo la kazi kiujumla kila
siku. Mtu anayetunza muda sifa yake huwa haipotei hata kwa watu wa mbali
na yeye.
Siri ya Sita:
Kuwa na Nidhamu ya Kutosha ya Matumizi ya Fedha.
Suala la kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha limenenwa sana na watu
wengi katika vitabu mbali mbali vilivyoandikwa. Waandishi wengi wa
vitabu vya kibiashara na maendeleo ya mtu binafsi wamejaribu kulisema na
kulielezea suala hili kwa ufanisi na ujunzi mkubwa ili kuwasaidia watu
kuweza kuwa na mafanikio makubwa katika eneo la uchumi na fedha. Ukisoma
vitabu mbali mbali vya fedha kama vile Total Money Makeover, The secret
of millionaire mind, Rich Dad Poor Dad, The Richest Man in Babyloan,
nakadhalika, Utajifunza mengi zaidi na kuona msisitizo waliojaribu
kuuweka juu ya kumsaidia mtu kufanikiwa kifedha.
Nami kwa makala yangu niliyowahi kutoa katika mtandao wetu mahali
hapa CICBAT, niliwahi kuzungumzia juu ya suala hili la matumizi ya
fedha. Hebu kwa kujifunza zaidi juu ya eneo hili ni vyema usome makala
hii; Fanya hivi kama unataka kufanikiwa katika matumizi mazuri ya fedha zako.
Siri ya Saba:
Kujenga tabia ya Kujiamini na Kujikubali binafsi.
Ni moja ya siri kubwa ambayo watu wengi hawaitambui na wengine
kuitambua lakini kutoitilia maanani katika utekelezaji wake. Kujiamini
ni hali ya kipekee inayokuwa ndani ya mtu kwa kujenga ujasiri pasipo
uogo juu ya kufanya au kutekeleza jambo fulani analolikabili mbele yake .
Huku pia Kujikubali ni sehemu inayomfanya mtu kujiona wa tofauti au
kipekee katika mazingira ya kile anachokifanya au kutaka kukifanya.
Hivyo tambua mambo yote hayo mawili yanaenda pamoja pasipo jambo moja
kuacha jingine. Ni vyema kabisa uwe na tabia ya kujifunza kujiamini na
kujikubali kama kweli unahitaji kufanikiwa na kufikia ndoto na malengo
yako makubwa uliyonayo hapa duniani. Huwezi kufanikiwa kamwe kama hauna
tabia ya kujiamini na kujikubali katika jambo lolote unalotaka kulifanya
au unalolifanya. Tabia hizi mbili huleta tabia ya UDHUBUTU, yaani tabia
ya kujaribu kufanya jambo pasipo uoga wowote ndani yako.
Katika kufahamu jambo hili zaidi hebu soma makala hii; Sababu moja ni hii, kwa nini hadi sasa umeshindwa kuanza biashara.
Hizo ndio siri muhimu za maisha ya mafanikio ya mtu binafsi hasa
katika kufikia mafanikio makubwa juu ya ndoto yake ya maisha. Ushauri
wangu kwako ni muhimu kila unaposoma makala moja kama hii ujifunze
kuweka kwenye matendo haraka (immediately) yale yote uliyoyasoma mahali
hapa. Kwa kufanya hivyo itakusaidia zaidi kufanikiwa haraka katika
malengo na mipango yako yote uliyojiwekea maishani mwako.
Hadi kufikia hapo sina jambo la ziada; nakutakia siku njema na maisha
mema ya mafanikio na baraka kwako, na zaidi sana uweze kuifikia ndoto
yako ya maisha uliyonayo.
Post a Comment