0

Image result for serikali ya tanzania

 
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) linatoa tahadhari kwa Wamiliki na Wakuu wote wa Vyuo vya Elimu ya Ufundi nchini kuwa kumeibuka matapeli wanaowaomba fedha au rushwa wakuu wa vyuo hasa vilivyopewa notisi na Baraza ya kushushwa hadhi au kufungiwa ili kuweza kuwasaidia kutatua matatizo yao kupitia namba mbalimbali za simu wanazozitoa.

Baraza linaendelea na kuwatahadharisha wateja wetu kuwa msikubali kupokea simu zenye kuwaomba fedha au kutoa kitu chochote wakati mnapotekeleza maelekezo ya Baraza au hata baada ya kutekeleza maelekezo hayo.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza anatoa tahadhari hii baada ya ofisi yake kupokea malalamiko hivi karibuni kutoka kwa baadhi ya Wakuu wa Vyuo na Wamiliki ambao wamedai kupigiwa simu na watu wanaojitambulisha kuwa Maafisa wa NACTE na kuwadai kiasi cha fedha kama masharti ya kutatuliwa matatizo yao. Pia Baraza limepokea taarifa kutoka kwa Wadau wanaolalamika kuwa kuna kundi la watu wanaodai kupewa fedha ili wasaidiwe kupangiwa vyuo fulani vya ufundi kwa masomo mbali mbali.

Baraza halina utaratibu wa kuomba fedha au zawadi ya aina yeyote kwa Mkuu wa Chuo au Mtu yoyote kama sharti la kupata huduma/msaada fulani.

Ni imani yetu kwamba wakati Baraza likiendelea na uchunguzi wa kuwabaini matapeli hao ili kuwachukulia hatua za kisheria, Wadau wetu wataongeza umakini na kuchukua tahadhari binafsi na watu wa namna hiyo.

Imetolewa na
Ofisi ya Katibu Mtendaji – NACTE
01 Septemba, 2016.

Post a Comment

 
Top