Serikali ya Sudan imefanya mashambulizi 30
yanayoshukiwa kuwa ya silaha za sumu katika eneo la Jebel Marra jimboni
Darfur tangu Januari mwaka huu ikitumia kile watalaamu wamesema ni
kemikali ya kusababisha malengelenge
Amnesty International imekadiria kuwa karibu watu 250 huenda
walifariki kutokana na silaha za kemikali. Shambulizi la karibuni kabisa
lilifanyika Septemba 9 na Amnesty imesema uchunguzi wake ulizingatia
picha za satelaiti, mahojiano na zaidi ya watu 200 na watalaamu
kuchunguza picha zilizoonyesha majeraha.
Mkurugenzi wa utafiti wa
migogoro wa shirika la Amnesty International Tirana Hassan amesema
matumizi ya silaha za sumu ni uhalifu wa kivita ""wakati wa mashambulizi
haya, mamia ya raia walipigwa risasi, maelfu walipoteza makaazi, na
moja ya mambo yanayokasirisha zaidi katika mgogoro wa Darfur ni kuwa
tumepata ushahidi wa kuaminika kuwa serikali ya Sudan imekuwa ikitumia
silaha za sumu dhidi ya raia"
Balozi
wa Sudan katika Umoja wa Mataifa Omer Dahab Fadl Mohamed amesema katika
taarifa kuwa ripoti hiyo ya Amnesty "haina msingi wowote kabisa” na
kuwa Sudan haimiliki aina yoyote ya silaha za sumu. Amnesty imesema
iliwakabidhi matokeo ya uchunguzi wake kwa watalaamu huru wa silaha za
sumu. "tuliwapa watalaamu huru wawili ushahidi wote tuliokusanya.
Waliuangalia na wakasema kuna ushahidi wa kuaminika kuwa kumekuwa na
matumizi ya aina Fulani ya kemikali na hasa, kuna uwezekano mkubwa wa
matumizi ya kemikali ya kusababisha malengelenge"
Sudan ilijiunga katika Makubaliano ya Silaha za Sumu mwaka wa 1999 ambapo wanachama hukubali kutotumia silaha za sumu.
Jeshi
la kulinda amani la Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, linalofahamika
kama UNAMID, limekuwa Darfur tangu mwaka wa 2007. Usalama bado ni tete
jimboni humo, ambapo makabila yasiyo ya waarabu yanapigana na serikali
ya Khartoum inayoongozwa na waarabu, na serikali inajitahidi kuyadhibiti
maeneo ya mashambani. Karibu watu 300,000 wameuawa Darfur tangu mzozo
huo ulianza 2003, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, wakati watu milioni
4.4 wanahitaji msaada na wengine milioni 2.5 wamepoteza makaazi.
Mahakama
ya Kimataifa ya Jinai ilitoa waranti za kukakamatwa Rais wa Sudan Omar
Hassan al-Bashir mwaka wa 2009 na 2010 kwa tuhuma za uhalifu wa kivita
na mauaji ya halaiki kutokana na operesheni yake ya kuangamiza uasi wa
Darfur.
Post a Comment