WAZIRI
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameitaka
Bodi mpya ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kupangua Menejimenti na
wafanyakazi waliomo katika shirika hilo kwa kuwa waliopo
hawajamridhisha.
Alisema
hajaona mabadiliko yoyote waliyoyafanya Menejimenti na wafanyakazi wa
kampuni hiyo na kuagiza Bodi hiyo kufanya mabadiliko katika muda wa
miezi mitatu kwa kubadilisha wote au kuacha wachache na kuchukua wapya.
Profesa
Mbarawa aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akizungumza na Bodi
hiyo yenye wajumbe sita wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Emmanuel
Korosso na Mkurugenzi wa ATCL, Ladislaus Matindi walioteuliwa na Rais Dk
John Magufuli Septemba 15, mwaka huu.
Alisema
mategemeo ya serikali kwa shirika hilo ni kuhakikisha wanaboresha mfumo
wa biashara kutoka wa zamani kwenda wa kisasa kutokana na usafiri wa
anga kuwa na ushindani mkubwa kibiashara.
‘’Tutakuwa
na Mikataba ya Ufanisi wa Kazi kati yangu na Mwenyekiti wa Bodi, Katibu
Mkuu, Mtendaji Mkuu pamoja na watendaji na wafanyakazi wote akiwemo
rubani, injinia na mkata tiketi. Mkataba huu utakuwa wa miezi sita na
kama kutakuwa na mtu ameshindwa kufanya kazi kwa ufanisi ataondolewa au
ajiondoe mwenyewe,’’ alisema Profesa Mbarawa.
Pia
alisema watendaji katika shirika wanatakiwa kuwa waadilifu kwani kwa
muda mrefu ATCL hakuna uadilifu, hali ambayo inachangia kutofanikiwa
katika mikakati yake ya kibiashara.
Aliongeza
kuwa Bodi hiyo inatakiwa kusimamia wafanyakazi na kwamba mtu yeyote
asiye na uadilifu aondoke mapema. Hata hivyo, alisema kuwa ATCL
inazaliwa upya hivyo ni lazima watendaji wawe na kasi kwani serikali
yenyewe imesimamia ununuaji wa ndege mbili kwa muda mfupi na
imefanikiwa.
Kwa
mujibu wa Profesa Mbarawa, ubunifu katika biashara ni nyenzo muhimu na
kwamba shirika hilo haliwezi kufika wanapotaka wasipokuwa wabunifu.
Aidha,
aliibua madudu yaliyokuwa yakifanywa na watendaji wa shirika hilo
kwamba kumekuwa na wizi wa mafuta ya ndege, abiria kusafirisha mizigo
bila kulipia.
Akitoa
mfano alisema abiria wa kwenda Comoro wamekuwa wakipakia mizigo mikubwa
kwenye ndege ya shirika hilo bila ya kulipia na hata wakilipia mapato
yanakuwa madogo, hivyo Bodi hiyo ihakikishe inayafanyia kazi suala hilo
haraka. Pia alisema kuna wakati abiria ambao walikuwa wakisafiri kwa
ndege hiyo, wanaambiwa siti zimejaa wakati zipo wazi.
‘’ATCL
imekuwa ikikabiliwa na upotevu wa fedha, nasisitiza kuwa iwekwe mifumo
imara, makini na mahiri katika kusimamia upotevu huu ili shirika letu
tunalolifufua liweze kukua,’’ alisema.
Katika
hatua nyingine, Waziri huyo alisema serikali inategemea kununua ndege
mbili aina ya jet mwakani baada ya ndege moja aina ya Bombardier Q 400
kutua nchini Jumanne wiki hii huku nyingine ikitarajiwa kutua Jumatatu
ijayo.
Alisema
Serikali inatambua changamoto ya madeni wanayodaiwa ATCL na kwamba
itafanyia kazi changamoto hiyo huku ikitarajia miezi miwili ijayo kutoa
maelekezo namna ya kuzipata ndege za jet.
Pia
alisema kuwa nauli ya ndege hizo mbili zitakazoanza kazi karibuni,
zitatajwa na kwamba zitakuwa nafuu kama ilivyo kwa ndege nyingine
tofauti na taarifa zinazosambaa mitandaoni. Kwa upande wake, Mwenyekiti
wa Bodi hiyo, Korosso alisema kuwa watahakikisha wanakuwa na mikakati ya
kibiashara yenye tija kwa kampuni hiyo.
‘’Tutayatekeleza
maagizo tuliyopewa na Waziri kwani hayana mjadala na tunaahidi
kuyafanyia kazi kwa haraka. Tunachokifanya sasa ni kulitambua kwa undani
shirika hili,’’ alisema Korosso.
Wajumbe
waliochaguliwa katika Bodi hiyo ni Dk Neema Munishi Mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliyebobea katika Menejimenti ya
Kimataifa ya Utawala Bora na Ibrahim Mussa ambaye ni Mkurugenzi wa
Utalii na Masoko kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Wengine
ni Mhadhiri wa UDSM, Dk Omary Mbura aliyebobea katika Fani ya Biashara
na Masoko, Dk Mussa Mgwatu ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa
Ufundi na Umeme (TEMESA) na Leonard Chimagu, Meneja wa Wakala wa Taifa
wa Barabara (TANROADS) mkoani Dodoma.
|
Post a Comment