|
SPIKA wa
Bunge, Job Ndugai amerejea bungeni kwa mara ya kwanza baada ya miezi
kadhaa ya kuwa nje ya nchi akitibiwa, na kuwarejesha ndani ya ukumbi
wabunge wa Upinzani, lakini akawaambia watunga sheria hao kuwa
wanatakiwa kuwa na umoja, ustahimilivu, busara, hekima, kuzingatia
Kanuni na Sheria pamoja na lugha zenye staha.
Alitumia
fursa hiyo kuwaasa wabunge kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia busara,
hekima, ustahimilivu na umoja huku wakitakiwa kujenga hoja ushawishi na
matumizi ya lugha zenye staha wakati wa vikao vya Bunge ili kujiepusha
na mihemko ndani ya Bunge.
“Nawasihi
kusoma na kuelewa hoja zinazoletwa mbele yetu ili kuzifanyia maamuzi
yaliyo sahihi,” alisema Ndugai ambaye alikuwa akitibiwa India.
Alimshukuru
Mungu kwa uponyaji na kumuwezesha kurudi tena nyumbani na bungeni
kuongoza Mkutano wa Nne wa Bunge la 11 ulioanza jana mjini hapa,
uliohudhuriwa na wabunge wa Kambi ya Upinzani waliokuwa wamesusa vikao
vya Bunge la Bajeti Juni mwaka huu.
Ndugai
pia alimshukuru Rais John Magufuli kwa kufuatilia matibabu yake na afya
yake kwa ujumla, wabunge, viongozi wa dini, na wananchi kwa kumuombea
wakati wote alipokuwa akipitia mapito ya kuugua.
“Niwashukuru
wapigakura wangu wa Kongwa kwa kuniombea na hasa baada ya kupata
taarifa za kushtusha kuwa mbunge wenu sipo tena duniani, lakini
nawashukuru kwa uvumilivu wenu,” alisema mbunge huyo wa Kongwa mkoani
hapa.
Wakati
Spika akishukuru na kurudi salama bungeni, wabunge wa upinzani (wa vyama
vinavyounda Ukawa) wakiongozwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani,
Freeman Mbowe wamerejea bungeni na kuungana na wabunge wenzao kuendelea
na shughuli za Bunge.
Akiendelea
kutoa taarifa ya Spika, Ndugai alimshukuru pia daktari kiongozi
aliyemtaja kwa jina moja la Dk Vijay kwa kuongoza matibabu yake
aliyeshirikiana na mkewe, Dk Fatma na kuongeza kuwa ni ukweli
usiopingika wanawake wanaweza.
Aliwashukuru
viongozi wanaosimamia shughuli za Bunge kwa kuongoza vizuri Bunge la
Bajeti la siku 70 lililoanza Aprili 9 hadi Juni 30, mwaka huu.
Alimpongeza Naibu Spika Dk Tulia Ackson kwa kazi nzuri wakati hayupo na
kwamba ni ya kupigiwa mfano.
Spika
aliwapongeza wenyeviti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, Andrew Chenge na
Najma Murtaza Giga na kuwataka waendelee kumpa ushirikiano kama
walivyoshirikiana wakati hayupo.
Tofauti
na matarajio ya wengi, hali ya amani na utulivu ilitawala bungeni licha
ya ujio wa wabunge wa upinzani ambao walisusa Bunge kwa takribani mwezi
mmoja hadi Juni 30, mwaka huu wakati wa Bunge la Bajeti lilipomaliza
vikao vyake.
Mbali ya
Mbowe, wengine waliokuwepo ni pamoja na Godbless Lema, Mchungaji Peter
Msigwa, David Silinde, John Heche na wengineo. Katika hatua nyingine,
Spika Ndugai alisema katika Mkutano wa Tatu miswada mitano ilipitishwa
na kwamba Rais John Magufuli ameshaisaini na kupitishwa kuwa sheria.
Alizitaja
sheria hizo kuwa ni Sheria ya Fedha na Matumizi ya Mwaka 2016, Sheria
ya Fedha Namba 2 ya Mwaka 2016, Sheria ya Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali Namba 3 ya 2016, Sheria ya Marekebisho ya Pili Namba 4 ya
2016 na Sheria ya Marekebisho ya Ununuzi wa Umma Namba Tano, 2016.
Post a Comment