0

Arusha. Sakata la posho za madiwani katika Jiji la Arusha limekuwa shubiri kwa madiwani baada ya kiwango walichokuwa wakipokea cha Sh60,000 kwa nauli za kuhudhuria vikao vya kisheria kupunguzwa hadi Sh10,000 na kuzusha mabishano.

Pia wametakiwa kurejesha fedha walizolipwa kwa mawasiliano ya simu Sh150,000 kwa mwezi tangu Novemba mwaka 2015 hadi Agosti mwaka huu, ambazo ni sawa na Sh40.8 milioni lasivyo, Sh50,000 zitakatwa kila mwezi kutoka kwenye posho zao.

Katika kikao cha baraza la madiwani  kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Shule ya Msingi Arusha, hoja kuhusu posho ilitawala baada ya Meya wa jiji hilo, Kalist Lazaro kutoa ufafanuzi kuwa zimekuwa zikitolewa tangu mwaka 2008 wakati wajumbe wengi wakiwa wa CCM, hivyo kushangazwa na ukubwa wake kwa sasa wakati baraza hilo likiongozwa na Chadema.

Kikao hicho kilichoanza saa 4:30 asubuhi hadi saa 3:43 usiku kilivunja rekodi ya vikao kufanyika kwa muda mrefu zaidi kutokana na majibizano. Baadaye baraza hilo  lilikaa kama kamati kutoa azimio dhidi ya mkurugenzi wa jiji baada ya kumtuhumu kukiuka kanuni naye akisisitiza anazifuta kikamilifu.

Lazaro amesema hakutakuwa na mabadiliko ya nyongeza au punguzo kwa stahiki za madiwani zilizoidhinishwa kisheria kuwawezesha kutimiza wajibu wao.

Post a Comment

 
Top