MWINJILISTI
wa Kanisa la African Inland Church (AICT), Charles Kazereng'wa (45),
amejinyonga hadi kufa, baada ya kumuua mwanaye, Malita Charles (15) kwa
kumpiga akimtuhumu kujihusisha na ufuska. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Geita, Mponjoli Rodson amelithibitishia gazeti hili kutokea kwa matukio
hayo juzi jioni.
Hata
hivyo, alisema kuwa asingeweza kulizungumzia suala hilo kwa undani kwa
sababu alikuwa kwenye sherehe za uzinduzi wa Wiki ya Nenda kwa Usalama
Barabarani ambayo kitaifa inafanyika mkoani Geita.
Hata
hivyo, habari za uhakika kutoka katika Kitongoji cha Elimu, Kijiji cha
Kaseme kilichopo wilayani Geita ambako mwinjilisti huyo alikuwa akiishi
na familia yake zinasema kuwa alichukua uamuzi wa kumwadhibu binti yake
huyo aliyehitimu darasa la saba mwaka huu, baada ya kumkuta akizungumza
na mwanamume ambaye hata hivyo hakufahamika.
Inaelezwa
kuwa baada ya kumpiga, alimchukua na kwenda naye nyumbani na kumfungia
ndani huku akiendelea kumwadhibu hadi alipofikwa na umauti.
Kwa
mujibu wa shuhuda ambaye hakuwa tayari kutajwa jina gazetini, baada ya
mwinjilisti huyo kubaini kuwa amemuua mwanaye, alichukua uamuzi wa
kukimbia umbali ya kilometa moja na kujitundika mtini kwa kamba
iliyomnyonga hadi kufa.
Kamanda
Mponjoli, alisema kuwa uchunguzi wa Polisi na wa madaktari unaendelea
na kwamba utakapokamilika miili ya marehemu wote wawili itakabidhiwa kwa
ndugu kwa ajili ya maziko.
Aliitaka
jamii kuwa makini wakati wa kuadhibu watoto kwa kuwa si wakati wote
wanapaswa kupewa adhabu kali na hatarishi kama vipigo vinavyoweza
kuwasababishia umauti.
Wakati
huohuo, baadhi ya wakazi wa Kata ya Kaseme wanaomfahamu mwinjilisti
huyo walieleza kwa nyakati tofauti kushangazwa na hatua aliyoichukua kwa
sababu hakuwa na tabia ya uhalifu wa aina yoyote wala ukatili.
Masaga
Makanika na Magesa Masai kila mmoja kwa wakati wake alisema kuwa
mwinjilisti huyo alikuwa ni muumini mzuri wa dini asiye na rekodi mbaya
ya matukio ya kiuhalifu na kwamba hatua alizochukua zimewaacha na
maswali mengi huku wakifikiri kuwa pengine ni mipango ya Mungu au
majaribu ya shetani.
Post a Comment