0

NA KENNETH NGELESI,MBEYA

BARAZA la madiwani la Halimashauri ya Mbeya limewafukuza kazi watumishi watatu kwa tuhuma za ubadhilifu katika zaidi ya shilingi milioni 500 zilizotolewa kwa ajili ya utengenezaji wa madawati na miradi ya maji katika Halmashauri.

Kadhalika, madiwani hao wamemvua madaraka na kutoa onyo kwa watumishi wengine kutokana na kushindwa kutekeleza na kusimamia majukumu yao kwa mujibu wa taratibu na muongozo wa kazi zao.

Akitangaza uamuzi huo jana kwenye kikao cha baraza la madiwani, ikiwa ni muda mfupi baada kujigeuza kama kamati, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mwalingo Kisemba, alisema hatua hiyo imetokana na mapendekezo ya tume ya uchunguzi baada ya Mkaguzi wa ndani kuibua hoja .

Aliwataja watumishi hao watatu waliofukuzwa kazi kuwa ni Mweka hazina wa Halmashauri hiyo, Hafidhu Mgagi, Ofisa elimu Msingi, Beth Mlaki, pamoja na Eliada Misana ambaye ni Kaimu Ofisa Ugavi.


Alisema watumishi hao walibainika kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maji na utengenezaji wa madawati,zikiwemo pia fedha za mishahara ya walimu.

“Kamati ya fedha iliunda tume ya kuchunguza tuhuma mbalimbali za ubadhirifu wa fedha za umma ambazo miongoni mwake zilikuwepo fedha za mishara ya walimu kiasi cha shilingi milioni 115 ambazo hazikulipwa kwa wahusika mwezi Aprili mwaka huu”  alisema Kisemba.

Aliongeza kuwa fedha nyingine zilizofanyiwa ubadhirifu ni za miradi ya maji kiasi cha shilingi milioni 400 ambazo zililipwa kwa wakandarasi kinyume na taratibu za manunuzi, ikiwemo kukosekana vielelezo vya malipo.

Aidha, Mwenyekiti huyo alisema katika uamuzi huo, baraza la madiwani limemvua madaraka Mhandisi wa Maji, Lovely Ng’ambi kwa kushindwa kutimiza majukumu yake, huku likimpatia onyo Kaimu Mhandisi wa Ujenzi, Edwin Magiri kutokana na kushindwa kuwajibika ipasavyo,

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Amelchiory Biyego, alisema amepokea uamuzi huo na  kwamba hatua inyofuata ni yeye kuhakikisha kama taratibu zilizotumika zimefuata utaratibu na miongozo ya uendeshaji wa Halmashauri.

Hata hivyo,  Mkuu wa Wilaya hiyo, Paul Ntinika  aliviagiza vyombo vya uchunguzi kuingilia kati suala hilo ili vifanye uchunguzi na wale wote watakaobainika waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Post a Comment

 
Top