0
MASHAKA Marwa (20), Mkazi wa Mtaa wa Ronsoti, mjini Tarime, mkoani Mara, amehukumiwa kwenda jela miaka 30 na kuchapwa viboko sita baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi mwanafunzi wa miaka 13 wa Shule ya Msingi Sabasaba.


Marwa ambaye ni mfyatua matofali, alimbaka mwanafunzi wa darasa la sita ambaye jina limehifadhiwa na kumsababishia maumivu makali huku akimwambukiza ugonjwa wa kisonono.

Akisomewa hukumu hiyo, Septemba 19 mwaka huu na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Tarime, Amon Kahimba, hakimu huyo alisema kwamba ameridhika bila shaka yoyote na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka uliokuwa na mashahidi sita akiwamo mwanafunzi huyo.

Pamoja naye alikuwapo babu yake, Siongo Marwa, fomu ya hospitali namba tatu, mganga aliyemhudumia mlalamikaji na mpelelezaji wa kesi hiyo, ambapo kwa upande mtuhumiwa hakuleta ushahidi mwingine wa kumuunga mkono, zaidi yake kuwapo yeye mwenyewe.

Awali, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Mwanri Mrisho, alidai kuwa mtuhumiwa Mashaka Marwa, mnamo Machi 12, mwaka huu, saa 9 mchana, mwanafunzi wa kike jina limehifadhiwa, wa darasa la sita katika shule ya msingi Sabasaba, akiwa nyumbani kwa babu yake, Siongo Marwa, anayeishi mtaa wa Ronsoti, alikwenda kujisaidia katika shamba la mahindi la babu yake, baada ya choo yao kubomoka.

Wakati akijisaidia alivamiwa na kushikwa shingoni kwa nyuma na mtuhumiwa, Mashaka, ambaye alimpiga ngwala na kumwangusha huku akimtishia kumuua kwa kumchoma kisu.

Marwa alianza kumnajisi mwanafunzi huyo ambaye alipiga kelele za kuomba msaada bila mafanikio. Mtuhumiwa huyo alitoroka baada ya kutenda unyama huo.

Mwendesha Mashitaka huyo wa Polisi, alidai kuwa baada ya mwanafunzi huyo kunajisiwa alikwenda kwa babu yake na kumweleza, wakaongozana naye hadi shambani kwake na kukuta mahindi yamevunjwa wakati wa purukushani za kumnajisi mwanafunzi huyo.

Babu yake alimchukua mjukuu wake hadi kituo cha Polisi na kupatiwa fomu ya matibabu namba tatu na kuongozana na askari wa kike hadi hospitali ya wilaya ambapo mwanafunzi huyo alifanyiwa uchunguzi na kukutwa amenajisiwa na kuambukizwa kisonono na akaanza kupatiwa matibabu.

Mtuhumiwa alijitetea na kudai kuwa ameshitakiwa kutokana na mgogoro wa ardhi na viwanja kati ya babu wa mwanafunzi huyo, Siongo Marwa na mzazi wake ambaye ni mama yake mzazi na kuiomba mahakama kumsamehe huku akidai amefungwa kutokana na mgogoro huo na kuomba nakala ya hukumu kwa ajili ya kukata rufaa.

Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Mwanri aliiomba mahakama kumpa adhabu kali kwani amemharibu mwanafunzi huyo na kumwambukiza ugonjwa wa zinaa ambapo Hakimu Kahimba alidai kuwa mshitakiwa angepeleka mahakamani ushahidi unaoonesha kuwa kuna migogoro ya ardhi.

Kwa bahati mbaya, hata mzazi wake hakufika mahakamni kutoa ushahidi hali iliyoonesha huenda alitaka kujiokoa kwa kutumia kisingizio cha migogoro ya ardhi.

Hivyo alimhukumu kwenda Jela miaka 30 na kuchapwa viboko sita na siku akitoka gerezani atamlipa mlalamikaji fidia ya Sh milioni nne ili liwe fundisho kwa wengine.
CHANZO-HABARILEO

Post a Comment

 
Top