0

Dar es Salaam. Wanafunzi 269 kati ya 290 waliotimuliwa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) mapema mwaka huu na ambao waliomba kuendelea na masomo ya ualimu, sasa watapelekwa kusomea ualimu wa shule za msingi, lakini watajilipia ada kulingana na viwango vilivyowekwa na Serikali.

Lakini mwezi uliopita, Serikali iliwarudisha wanafunzi 382 kuendelea na kozi hiyo ya masomo ya sayansi na hisabati baada ya kuthibitisha kuwa walikuwa na sifa.

Siku hiyo, Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako alisema wanafunzi wengine 4,586 wa mwaka wa kwanza wa programu maalumu wa stashahada ya ualimu wa sekondari waliokidhi vigezo vya ufaulu, wangehamishiwa vyuo vya ualimu na wengine 1,337 wa mwaka wa pili wangehamishiwa vyuo vya Korogwe na Kasulu ili kumalizia masomo yao.

Profesa Ndalichako alisema wanafunzi wengine 29 wa mwaka wa pili ambao wana cheti cha daraja A la ualimu, wangehamishiwa Chuo cha Ualimu Kasulu ili wamalize masomo yao ila kwa gharama zao, huku wengine 1,181 wakitakiwa waombe nafasi kwenye vyuo vingine kwa masomo ambayo wana sifa zinazostahili.

Jana, naibu katibu mkuu wa Wizara ya Elimu, Dk Leonard Akwilapo alisema Serikali imeamua kuwarejesha wanafunzi hao 269 kwenye vyuo vyake, lakini kusomea ualimu wa elimu ya msingi.

Alisema awali Serikali iliagiza wanafunzi hao waombe mafunzo watakayoona yanawafaa kulingana na ufaulu wao, lakini baada ya kutafakari kwa kina kupokea maombi kutoka kwao imeridhia kuwapanga katika vyuo vyake.

Post a Comment

 
Top