0

RAIS John Magufuli ameutaka uongozi wa Jiji na Manispaa za Dar es Salaam kutowaondoa wafanyabiashara ndogo ‘machinga’ katika maeneo waliyopo hadi watakapowatengenezea utaratibu mzuri wa kufanya biashara zao.

Akizungumza na wanachama na wananchi waliojitokeza kumpokea wakati alipofika katika Ofisi Ndogo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam kwa ajili ya kuingia kwenye ofisi yake ya uenyekiti kwa mara ya kwanza, Rais Magufuli alisema umefika wakati watu wanatakiwa kubadilika.

Alisema wamejipanga kufanya kazi kwa niaba ya masikini kwa kuwa yeye hakuchaguliwa na matajiri, hivyo atasimama kwa ajili ya masikini kwa kuwa hata yeye ni mtoto wa masikini hivyo atatembea na masikini wenzake, alisema matajiri walipe kodi na masikini wasilipe kodi.

“Ninataka Dar es Salaam mpya, kwa hiyo hatua nyingine tunazozichukua wapo wengine wachache sana wanaweza wasizifurahie, naomba muwapuuze kwa sababu tunafanya kwa maslahi ya watu wa kawaida,” alisema.

Aliwataka viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam waanze kujipanga namna watakavyotengeneza mazingira mazuri kwa watu hao kufanya biashara zao. Alitoa mfano kuwa, haiingii akilini mtu kumtuma mgambo kwenda kumnyang’anya mama lishe chakula chake, jambo ambalo alisema ni dhambi kubwa.

Alisema anataka Tanzania ambayo masikini anakuwa na haki sawa na tajiri, huku akiwataka wafanyabiashara ndogo na wao kuzingatia sheria, kwani hawawezi kujipanga katika eneo moja.

Alisema kama watakuwa na vikundi vyao, wakajipanga vizuri watauza ili mradi wanaweka mazingira safi na si wanatengenezewa sehemu nzuri na wao waigeuze genge la vibaka na hata kufanya wateja wahofie kwenda.

Aidha, alisema kuna mchezo ambao unafanyika kwa wafanyabiashara hao kwenda kuchukua bidhaa kwa wauzaji wa bidhaa hizo na kuziuza mitaani na kumfanya mtu huyo kukwepa kodi wakati serikali inataka kukusanya kodi, hivyo ni muhimu wanaponunua bidhaa zao wakumbuke kudai kodi.

“Tunataka Dar es Salaam liwe jiji la biashara na ndio maana sisi tumeamua kwenda Dodoma, tunataka hapa pafanyike biashara za kimataifa, hivyo wenye kuweza kufanya wafanye. Ndio maana mimi na chama changu tuliamua kupeleka muswada wa kuifanya nchi yetu kuwa ya viwanda,” alisema Rais Magufuli.

Post a Comment

 
Top