Maisha si marahisi wakati wote kama wengi wanavyozani hasa pale
unapokutana na changamoto mbali mbali zinazoweza kuwa kizuizi kikubwa
juu ya jambo lako zuri unalotaka kulitimiza kwa wakati fulani. Kuna
wakati unaweza ukawa unatamani kukamilisha wajibu fulani mkubwa mbele
yako, ili uweze kufikia hatua ya juu ya kufanikiwa na kuleta matokeo
chanya katika maisha yako lakini hali ikawa tofauti na unavyotaka iwe
kwa kipindi hicho. Yawezekana unahitaji kuchukua hatua kwa ajili ya
kukamilisha malengo na mipango yako mizuri uliyonayo lakini kila
unapootaka kufanya hivyo unakosa msukumo na nguvu ya kuchukua hatua
husika.
Mambo mengi umeghairisha kwa sababu ya kukosa msukumo binafsi wa
kuchukua hatua za kivitendo na hatimaye umeshindwa kuleta matokeo chanya
katika maisha yako. Wapo watu wengi kila wanapojaribu kupanga jambo
fulani wanapanga vizuri, ila unapofika wakati wa kutaka kuchukua hatua
wanakuwa wanakosa msukumo na nguvu ya ndani ya kuwasaidia kutimiza
wajibu walionao ili kuleta matokeo na mabadiliko makubwa katika maisha
yao. Je, na wewe ni miongoni mwa watu wa namna hii? Soma makala hii ili
kuchukua hatua ya mabadiliko yako leo hii.
Hapa kuna mambo 10 yanayoweza kukusaidia ili kuondokana na hali ya namna hiyo.
1: Kubali tatizo.
Jambo la kwanza ili uweze kuondokana na hali ya kuchoka na
kutojisikia kuchukua hatua ya kivitendo juu ya malengo na mipango yako
uliyonayo ni kuamua kulikubali tatizo. Ndio. Kubali kuwa una tatizo la
kutokuchukua hatua za haraka na mara kwa mara kila unapotaka kufanya
hivyo, kwani unapokubali tatizo unatoa nafasi ya kulishugulikia hilo
tatizo kwa moyo wako wote hadi linaondoka.
2: Tengeneza ratiba na kuifuata kila siku.
Baada ya kukubali una tatizo la kutokuwa na wepesi wa kuchukua hatua
ni vizuri utengeneze ratiba yako maalum inayoweza kuwa msaada mkubwa
kwako kwa ajili kukupa mwelekeo katika majukumu yako ya kila siku.
Unapokuwa na ratiba au unapojiwekea vipaumbele vyako vya kufanya kila
siku unakuwa umejifunga mwenyewe binafsi kiakili na kifikra juu ya mambo
gani ya kufanya juu ya siku nzima uliyonayo mbele yako.
3: Tengeneza picha ya mafanikio yako unayohitaji.
Unapotengeneza picha halisi juu ya jambo fulani unalotaka kulitimiza
hii itakusaidia zaidi kukupa nguvu na msukumo mkubwa ndani yako hasa kwa
ajili ya kuchukua hatua za kivitendo pasipo hofu na uoga ndani yako.
Jifunze kuona mafanikio ndani yako kabla hayajawa halisi katika hali ya
nje hii ndio njia nzuri ya kukupa msukumo wa kipekee wa kutimiza malengo
na mipango yako yote uliyonayo.
4: Tafuta namna ya kujihamasisha mwenyewe.
Unapochukua hatua ya kujihamasisha mwenyewe binafsi unakuwa
unatengeneza nguvu mpya ndani yako itakayokufanya kupata msukumo wa
kuchukua hatua ya haraka ya kivitendo juu ya ndoto yako uliyoanayo.
Jifunze kujihamasisha kwa kupitia kusoma vitabu vinavyohusiana na fani
yako au kitu unachofanya, sikiliza mafundisho mazuri ya kukujenga na
kukupa hatua mpya, penda kuhudhulia semina na warsha mbalimbali za
kukujenga na kukusaidia katika kufikia ndoto yako.
5: Weka uzito juu ya jambo unalotaka kulifanya.
Ni vyema usisubiri mtu mwingine aje kwa ajili ya kukusaidia kuona
uthamani na uzito wa ndoto yako uliyonayo. Kama unataka kufanikiwa
kwenye kila jambo unalotaka kulichukulia hatua za kivitendo na
kulifanikisha kwa haraka, ni vizuri ujifunze kuweka uzito kwenye kila
jukumu ulilonalo mbele yako pasipo kujiwekea kizuizi cha hofu na mashaka
ya kulitekeleza. Fanya hivyo leo ili kuleta matokeo makubwa katika
maisha yako. Weka uzito kwenye kila jambo unalolifanya ili kuleta
matokeo makubwa yatakayowashangaza watu wengi.
6: Anza na hatua ndogo kwanza.
Wapo watu wengi kila wanapotaka kutimiza malengo yao na mipango
fulani waliyonayo huwa ni watu wa kusubiri wafanikishe kwanza hatua
fulani kubwa itakayoweza kuwaletea mafanikio ya haraka kabla hawajapita
kwenye hatua ndogo zinazoweza kuwa msingi mzuri wa kule wanapoelekea.
Anza kidogo kidogo kwa ulichonacho; anza kuchukua hatua ndogo leo hii
ili uweze kuleta matokeo madogo yanayoweza kuzaa njia mpya na pana ya
kukupeleka katika mafanikio mengine makubwa zaidi.
7: Furahia mafanikio madogo unayoyapata.
Usikubali kuishi ukisubiri ufanikishe kila kitu ndio uwe na furaha ya
kutosha maishani mwako. Jifunze kujenga furaha katika kila hatua
unayoipiga katika maisha yako, furahia hatua ndogo uliyoipiga katika
kufanikisha malengo yako uliyokuwanayo pasipo kusubiri hatua fulani ya
kiwango cha juu ili kuleta furaha unayohitaji ndani ya moyo wako.
Kumbuka furaha pia ni mojawapo ya chanzo cha mafanikio yako unayohitaji,
unapopoteza furaha ndani yako unakuwa unapoteza nguvu ya kusogea mbele.
8: Kubali changamoto na amua kusonga mbele.
Kama umeshindwa kufanikisha lengo lako moja usikubali kukata tamaa ya
kuchukua hatua kwenye lengo lako lingine ulilonalo maishani mwako. Amua
kukubali kila changamoto unayokutana nayo kwenye maisha yako na
kuikabili ili uweze kufanikisha ndoto yako uliyonayo, usikate tamaa
haraka kwa sababu hujafanikisha malengo mengine uliyokuwanayo, songa
mbele amini kwa bidii na juhudi yako utafanikiwa.
9: Tafuta mshauri wa karibu (mentor).
Unapokuwa na mtu wa kukushauri na kukusaidia kimawazo kila unapopitia
hali ngumu ya kukosa hamasiko la kuchukua hatua fulani katika malengo
yako, hii ni njia nzuri inayoweza kukuweka salama zaidi hasa katika
kukupa mwelekeo mpya na nguvu kubwa ya kusonga mbele kila wakati. Tafuta
mtu unayemwamini zaidi na anayeweza kuwa mshauri na mwelekezi mzuri
katika maisha yako katika kile kitu unachotaka kukifanikisha (life coach
or mentor).
10: Tafuta msaada kutoka kwa wengine.
Kumbuka kila mtu amepewa kipaji chake na uwezo wa kipekee ndani yake
unaokuwa tofauti na mwingine. Hivyo basi ni vizuri unapopitia katika
hali ya kuchoka au kutokujisikia kuchukua hatua fulani juu ya jambo
unalotaka kulifanikisha, ni vyema uamue kutafuta watu waaminifu wa
karibu yako kama vile marafiki unaowaamini, ndugu, wazazi, mshauri wako,
nakadhalika, ili waweze kukusaidia na kukutia moyo juu ya jambo
unalotaka kufanya. Amini unauwezo mkubwa ndani yako, chukua hatua leo
pasipo kuogopa na amini utafanikiwa katika jambo unalotaka kufanya.
JIAMINI NA AMINI UNAWEZA. ISHI NDOTO YAKO.
Post a Comment