0

Moja ya njia ambazo wafanyabiashara wanaweza kutumia kukuza biashara zao ni kuongeza mtaji. Ili kuongeza mtaji kuna mambo ambayo mfanyabiashara anaweza kufanya kama kuwekeza zaidi kwenye biashara yake, kupata ruzuku au kuomba mkopo.

 Mikopo ya kibiashara imekuwa rahisi kupatikana kwa sasa kuliko ilivyokuwa hapo nyuma. Hii inatokana na wingi wa taasisi zinazotoa mikopo hii, kuanzia benki mpaka watu binafsi sasa wanatoa mikopo ya kibiashara.

Wapo wafanyabiashara wengi ambao wanalalamika mikopo imeharibu biashara zao. Wengi walikuwa na biashara zinazokwenda vizuri na hivyo kushawishika kwamba wakichukua mkopo mambo yatakuwa mazuri zaidi. Kinyume na matarajio yao, wanachukua mkopo na biashara inayumba mno na hata kuelekea kufa.

Haya yote yanatokana na wafanyabiashara kuchukua mkopo bila ya kuzingatia mambo muhimu kuhusu mikopo ya kibiashara. Leo tutakwenda kujadili hili kwa kina ili unapokwenda kuchukua mkopo, uwe na uelewa na uweze kuutumia vizuri ili biashara yako iweze kukua zaidi.

Jambo la kwanza na muhimu kuzingatia ni matumizi ya mkopo wenyewe. Ukishaomba na kupata mkopo, huwezi kuutumia kama unavyojisikia wewe, au kwa sababu kuna changamoto fulani imetokea kwenye biashara yako basi unatumia fedha za mkopo kwa sababu unazo. Unahitaji kuwa na nidhamu kubwa kwenye matumizi ya mkopo wako.

Tumia mkopo uliopata kwa shughuli ile uliyodhamiria kuchukulia mkopo. Ni muhimu uzingatie hili kwa sababu kuna mambo mengi yanaweza kujitokeza na yakakushawishi utumie mkopo tofauti na ulivyopanga. Unaweza kutumia lakini mwishowe ukasumbuka kwenye kulipa mkopo huo.

Chukua mkopo na uweke kwenye kitu ambacho tayari kinazalisha. Usichukue mkopo na kwenda kujaribu kitu kipya kabisa, hasa kama ni mfanyabiashara mdogo. Hiki ni kitu kingine muhimu unachotakiwa kuzingatia unapochukua mkopo.

Unapochukua mkopo, unategemewa uanze kurejesha mkopo huo mapema iwezekanavyo, na njia pekee ya kurudisha mkopo huo na biashara yako ibaki salama, ni kuuweka kwenye eneo la biashara ambalo tayari linazalisha. Kwa njia hii utaongeza faida na hivyo kuweza kulipa mkopo wako.

Lakini kama utachukua mkopo na kwenda kuanza kitu kipya, utajikuta unatakiwa kuanza kulipa mkopo kabla hata hujaanza kupata faida, na hivyo kutoa fedha nyingine kwa ajili ya kulipa mkopo.

Usikuze mapato yako wala kupunguza matumizi yako. Wakati watu wanaomba mkopo, huwa wanapangilia mkopo huo kwa namna watakavyoutumia na mapato watakayotengeneza. Kwa hesabu hizi watu huona faida kubwa wanayoweza kupata kupitia mkopo wanaochukua. Ila hapo kuna tatizo moja, mara nyingi watu wanakuza mapato yao na kupunguza matumizi yao.

Hii inawafanya waone faida ni kubwa, lakini wanapokuja kwenye uhalisia, mambo yanabadilika. Ili uweze kwenda vizuri, fanya mahesabu ya uhalisia, kwa kuangalia sasa mambo yanakwendaje. Kuchukua mkopo hakubadilishi sana mambo yanavyokwenda sasa, hivyo ni vyema kuwa na mipango inayoendana na uhalisia ili usivunjike moyo.

Hakikisha unakuwa na fedha ya ziada baada ya kutumia mkopo uliochukua. Kitu ambacho wafanyabiashara wengi wamekuwa hawazingatii ni kuchukua mkopo wote na kuweka kwenye biashara, wanabaki hawana fedha ya ziada na hivyo kutegemea kuanza kuvuna faida.

Kama ambavyo kila mfanyabiashara anajua, changamoto hazikosekani kwenye biashara, matatizo ni sehemu ya biashara. Kwa mtu kuweka fedha zote kwenye biashara, inapotokea changamoto au tatizo, wanashindwa kulitatua kwa sababu fedha wanakuwa wameshatumia zote.

Kuepuka hili tumia theluthi mbili au robo tatu ya mkopo kwenye biashara yako, na ile inayobaki ikae kama fedha ya dharura, ambayo utaweza kuitumia pale changamoto itakapoibuka. Kwa njia hii, ni vyema ukachukua mkopo ambao unazidi kidogo yale matumizi uliyojipangia, ili uweze kubaki na kiasi cha dharura.

Kitu cha mwisho tunachokwenda kukumbushana hapa leo ni pale unaposhindwa kulipa mkopo kwa wakati, usikimbie wala kujificha. Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiharibu sifa zao za ukopeshwaji kwa kukimbia pale wanaposhindwa kurejesha mikopo yao.

Lakini kukimbia huko huwa hakuwasaidii na wakati mwingine kunawaletea hasara kubwa ikiwa ni pamoja na kufilisiwa. Unaposhindwa kulipa mkopo kwa wakati, rudi kwa waliokukopesha na ongea nao, eleza hali yako ilivyo na mnaweza kupanga upya namna ya kulipa mkopo huo. Unapoonesha nia hii na wao wanapata moyo kwamba unajali kuhusu mkopo uliochukua.

 Ila pale unapoanza kukimbia, ukitafutwa hupatikani, unajenga picha hasi na hivyo kuwafanya wachukue hatua za kisheria ili kupata fedha zao. Hakuna asiyekutana na changamoto, na dawa ya deni ni kulipa, hivyo omba upatiwe muda zaidi uweze kulipa mkopo uliochukua. Unapoingia kwenye hali hii ya kushindwa kulipa, kazana ulipe na jifunze kupitia hali uliyopitia.

Mkopo unapaswa kuwa kichocheo cha biashara yako kukua, zingatia haya tuliyojifunza ili uweze kutumia vizuri mkopo wa kibiashara unaochukua. Kila la kheri.

Post a Comment

 
Top