0

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda amekuwa Mkuu wa Mkoa wa tatu katika utawala wa Rais John Magufuli ‘kupigwa chini’ baada ya uteuzi wake kutenguliwa jana na nafasi hiyo kupewa aliyekuwa Mkuu wake wa Wilaya ya Arusha, Mrisho Gambo (34).
Ntibenda anaungana na Anne Kilango-Malecela na Magesa Mulongo, ambao uteuzi wao ulitenguliwa na Rais Magufuli. Kilango alikuwa mkoani Shinyanga na Mulongo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Gambo anaungana na wakuu wa wilaya wengine vijana, wakiwamo Paul Makonda (Dar es Salaam) na Anthony Mtaka (Simiyu).
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa vyombo vya habari jana, Gambo anatarajiwa kuapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam leo, wakati Ntibenda ambaye uteuzi wake umetenguliwa, anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu ambako atapangiwa majukumu mengine.
Nyota ya Gambo ambaye ni mmoja wa viongozi vijana nchini, ilianza kung’ara baada ya kugombea ubunge wa Afrika Mashariki Aprili 2012 na kushika nafasi ya sita kati ya wagombea 81.
Baadaye, mwezi Mei mwaka huo, aliteuliwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe. Hata hivyo, upepo mbaya wa kisiasa ulimpitia kiongozi huyo baada ya kuwa mmoja wa ma-DC ambao Kikwete alitengua uteuzi wao Februari 18, 2015.
Hata hivyo, Mei 10, 2015 jina la Gambo liling’ara tena, pale Rais Kikwete alipoteua majina ya wakuu wapya wa wilaya na alipangiwa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Katika uteuzi wa ma-DC wapya wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Magufuli, Julai mosi mwaka huu, jina la Gambo lilisikika tena baada ya kuwa miongoni mwa wakuu hao wapya wa wilaya, akipangiwa Wilaya ya Arusha.
Atoa ya moyoni
Baada ya uteuzi jana, Gambo alizungumza na kusema anamshukuru Mungu kwa kuteuliwa na Rais Magufuli kuongoza Mkoa wa Arusha.
Akizungumza kwenye mkutano wa kazi kwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa, uliofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Gambo alisema hana la kusema zaidi ya kumshukuru Mungu.
“Sikutarajia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, namshukuru sana Rais kwa uteuzi huu na naahidi kuwatumikia vyema wananchi wa Arusha sambamba na kushirikiana na wadau katika kuleta maendeleo. “Lakini zaidi namshukuru sana Mwenyezi Mungu sana kwa kuniwezesha rehema zake. Nafahamu fika kuwa Arusha ina changamoto nyingi lakini kwa uwezo wa Mungu nitaweza kuzikabili na kuzitatua,” alisema Gambo aliyezaliwa Mei 22, 1984 katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.
Wananchi wamzungumzia
Katika hatua nyingine, wananchi wa Arusha walisema jana kuwa uteuzi huo ni matokeo ya Rais kumuona mkuu huyo wa wilaya kuwa ni kijana mchapa kazi na asiyekuwa tayari kuyumbishwa na siasa na wanasiasa wasiozingatia weledi.
Wakizungumza na gazeti hili, wakazi hao wa Arusha akiwemo Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Catherine Magige (CCM) walisema wanamshukuru Rais Magufuli kwa kutambua mchango wa vijana katika ufanyaji wa kazi na kuhimili mikikimikiki wanayokutana nayo kwenye uongozi.
Magige alisema Gambo ni zao la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na kwamba mbali ya kuwa ni mwanasiasa, lakini amekuwa mstari wa mbele katika utendaji wa kuharakisha maendeleo ya wananchi na kutatua kero zao akishikilia nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha.
“Gambo alichaguliwa na Rais kwa nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha na sasa Rais kamuona na kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, hii ni ishara kuwa vijana wakipewa nafasi wanaweza kuonesha makubwa zaidi na watu wakashangaa. Tunashukuru Rais kwa hili na pia tunawasihi viongozi wachape kazi,” alisema.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Lengai ole Sabaya alisema kuteuliwa kwa Gambo ni ishara tosha ya kushangaza watu kuwa vijana wanaweza kuonesha uwezo wa hali ya juu, ikiwepo kupambana na changamoto wanazokumbana nazo wakati wa ufanyaji wa kazi zao.
Mkazi mwingine, Julius Lameck alisema Ntibenda alikuwa na mambo mbalimbali, aliyoyafanya na kuyaacha kama mfano hivyo mazuri yanapaswa kuchukuliwa na kuenziwa, ikiwemo kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa.
GAMBO NI NANI?
Alizaliwa Mei 22, mwaka 1982 katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Ilala Boma na kuhitimu darasa la saba mwaka 1997.
Alianza kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kibaha mkoani Pwani na kuhitimu kidato cha nne mwaka 2001. Mwaka 2002 alijiunga kidato cha tano Shule ya Ufundi Tanga, maarufu kama Tanga Technical School na kuhitimu kidato cha sita mwaka 2004.
Mwaka 2005 alichaguliwa kujiunga na Chuo cha Uhasibu Arusha kusomea Stashahada ya Juu katika Sayansi ya Kompyuta na kuhitimu mwaka 2008. Mwaka 2009 aliajiriwa kwa nafasi ya Mchambuzi wa Mifumo ya Kompyuta katika Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Mwaka 2011 aliajiriwa kama Msimamizi Mwandamizi wa Mifumo ya Kompyuta wa Chuo cha Kimataifa cha Nelson Mandela. Mwaka 2011 alijiuzulu nafasi hiyo Chuo cha Nelson Mandela na kurudi Halmashauri ya Jiji la Arusha. Aliweza kurudi Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kuwa hakuwa ameacha kazi, bali aliomba likizo bila malipo.
Mwaka 2010 alijiunga tena Chuo cha Uhasibu Arusha kusoma Shahada ya Uzamili katika masuala ya uongozi na teknolojia ya habari na kuhitimu mwaka 2011. Aprili 2012 aligombea ubunge wa Afrika Mashariki na kushika nafasi ya sita kati ya watu 81 waliogombea.
Mei 2012 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe. Julai 2016 aliapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, nafasi aliyokuwa akiishikilia hadi jana alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, kuchukua nafasi ya Felix Kijiko Ntibenda.

Post a Comment

 
Top