0
MKAZI wa kijiji cha Msati katika wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara, Bahati Hunga (39), amehukumiwa na Mahakama ya mkoa wa Mara kutumikia kifungo cha miaka 25 jela au kulipa faini ya Sh milioni 88, baada ya kupatikana na hatia ya kukamatwa na vipande sita vya meno ya tembo kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu, Adrian Kilimu baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na waendesha mashitaka wa serikali, Jonas Kaijage na Frank Nchanila kuwa, mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 24, 2014 akiwa na vipande sita vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh 800,000 katika eneo la kijiji cha Itiryo wilayani Tarime kinyume cha sheria.
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, waendesha mashitaka hao waliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa huyo ili kuwa fundisho kwake na kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo na adhabu hiyo inaunga mkono kaulimbiu ya serikali ya kuhakikisha wanyamapori wanalindwa kwa nguvu zote dhidi ya majangili.
Hata hivyo, mtuhumiwa huyo alipewa nafasi ya kujitetea na ndipo aliiomba mahakama hiyo kumpunguzia adhabu kwa sababu anayo familia inayomtegemea.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Kilimu alisema ameridhika pasipo kuacha shaka dhidi ya ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka na ndipo akamhukumu kifungo cha miaka 25 jela au alipe faini ya Sh milioni 88, ambako mtuhumiwa huyo alikosa faini hiyo na kwenda jela kutumikia adhabu hiyo.

Post a Comment

 
Top