Rais wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza kuwa shirika la ndege la Tanzania
litarejea angani ''kabla ya mwisho wa mwezi Septemba Mwaka huu 2016''.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na kaimu mkurugenzi wa mawasiliano ya ikulu ya Tanzania bw Gerson Msigwa
''Dkt. Magufuli amesema serikali yake imechukua hatua madhubuti za kulifufua shirika la ndege la Taifa.
Tayari
mipango imefanywa kuhakikisha ndege mbili aina Bombadier Q400
zinanunuliwa na zitatua hapa nchini kabla ya mwisho wa mwezi Septemba
Mwaka huu 2016.'' taarifa hiyo inaeleza.
Tamko hilo ni ishara
nzuri kwa sekta ya uchukuzi nchini Tanzania na vilevile kanda nzima ya
Afrika Mashariki ambayo imekuwa ikikabiliwa na gharama za juu za usafiri
kutoka kwa mashirika ya kigeni.
BIASHARA NA RWANDA
Wakati
huohuo rais Magufuli aliueleza ujumbe wa wafanyabiashara kutoka
Rwanda kuwa China imeonesha nia ya kushirikiana na Tanzania kujenga reli
ya kisasa yaani “Standard Gauge” kwa nia ya kurahisisha uchukuzi wa
mizigo kutoka bandari ya Dar es salaam kwa manufaa ya wafanyabiashara.
''Tanzania imeamua kuipatia Rwanda eneo la kujenga
bandari kavu kwa ajili ya mizigo ya wafanyabiashara wake na pia Mamlaka
ya Bandari Tanzania (TPA) itafungua ofisi mjini Kigali nchini Rwanda
ikiwa ni juhudi za kurahisisha na kuongeza biashara kati ya nchi hizi
mbili.''
Juhudi hizo bw Magufuli anasema ni kuwahakikishia
wafanyabiashara wa Rwanda kuwa bandari ya Dar es salaam ni salama kwao
kupitisha mizigo na ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea
kuchukua hatua za kuimarisha bandari hiyo na kurahisisha biashara kati
ya nchi hizi mbili.
Kwa upande wake rais Paul Kagame wa Rwanda
alitoa wito kwa ''Tanzania na Rwanda pamoja na nchi nyingine za Jumuiya
ya Afrika Mashariki kushirikiana na sekta binafsi katika kutumia fursa
nyingi za kibiashara zilizopo baina yake na kuwaletea manufaa
wananchi''.
Post a Comment