0

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kupungua kwa mizigo bandarini kumeathiri si Tanzania pekee bali dunia nzima na kwamba kubanwa kwa mianya ya wizi kumesababisha kuongezeka kwa mapato kutoka Sh bil 458 Aprili mwaka huu kufikia Sh bil 517.

Aidha, TRA imesema itaanza uhakiki wa namba za utambulisho wa mlipakodi (TIN) kutokana na kuwepo watu wenye namba mbili na wasiohakiki watalazimika kudaiwa kodi na TRA.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari jana, Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata alisema upungufu huo wa mizigo bandarini umezikumba pia bandari za Beira, Msumbiji, Mombasa, Kenya na kwingineko na kusababisha mapato kupungua.

“Lakini sisi pamoja na upungufu wa mizigo bandarini makusanyo yanazidi kuongezeka kutokana na kuzibwa mianya ya kukwepa kodi, hivyo napenda kuwapongeza wafanyakazi wote wa mamlaka na kusema kwa sasa hakuna mtu anayeweza kukwepa kodi na wale waliozoea wakae katika njia kuu,” alisema Kidata.

Kidata alisema wananchi wanatakiwa kuwaunga mkono kwani sasa kodi inaonekana katika kufanya shughuli za serikali kama kuboresha miundombinu pamoja na kutoa elimu bure.

Alisema TRA imefikia na kuvuka lengo la makusanyo ya kodi kwa mwaka wa fedha 2015/16 kwa kukusanya Sh trilioni 13.8 sawa na asilimia 100.04 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 13.4 iliyokuwa imepangwa na serikali.

Kidata alisema katika kipindi cha Juni mwaka huu, TRA imekusanya Sh trilioni 1.4 sawa na asilimia 107.83 ya lengo la kukuzanya Sh trilioni 1.3 ambapo makusanyo ya mwaka wa fedha 2015/16 ni sawa na ongezeko la asilimia 23.70 la makusanyo ya mwaka 2014/15.

Akizungumzia mashine za kielektroniki za EFDs, Kidata alisema walipoanza utoaji mashine hizo zilikuwa 5,703 na mpaka sasa mashine 1,700 zimegawiwa kwa watumiaji na wataanza kupita duka hadi duka kuhakiki matumizi ya mashine hizo.

Kamishna wa mapato ya ndani, Elijah Mwandumbya, alisema mwaka huu wa fedha wamejipanga kuhakikisha wanaondoa changamoto kwa mtu mmoja kuwa na TIN zaidi ya moja hivyo watafanya uhakiki.

“Ni vema wananchi kujitokeza ili wasibaki na TIN namba ambayo haitumiki kwani ukibaki nayo baadaye utadaiwa kodi,” alisema Mwandumbya.

Akizungumzia matumizi ya mashine za kielektroniki za EFDs alisema katika kuhakikisha nchi inakuwa na mfumo wa matumizi ya mashine hizo watapita katika maduka na nyumba kwa nyumba kuhakikisha kila mfanyabiashara kama anatumia mashine hizo.

Mwandumbya alivikumbusha vituo vyote vya mafuta kuhakikisha wanatumia mashine hizo ifikapo Oktoba mosi mwaka huu.

Alisema wanaandaa vituo vipya vya kutoa huduma ya ulipaji kodi kuondoa misongamano ya watu.

Akifafanua zaidi kuhusu vituo vipya, alisema wameandaa kituo kipya cha Millennium Tower na maandalizi yanaendelea kufungua vituo vingine Ubungo Plaza na katika eneo la barabara ya Nyerere.

Naye, Kamishna wa walipa kodi wakubwa, Neema Mrema alitoa onyo kwa wafanyabiashara wakubwa watakaobainika kutumia mashine za risiti za kughushi za EFDs kuwa watalipa kodi walizokwepa na faini.

Post a Comment

 
Top