Maneno yako ndio yanaonyesha wapi unapoelekea, na vitendo vyako
vinaleta uhalisi wa kile ulichokipanga. Hivyo basi, kumbe kwa maneno ya
kinywa cha mtu unaweza kutambua mtu atakuwa wapi kwa miaka mitano badae,
na kwa uamuzi wake wa kuchukua hatua ya utekelezaji utaona kwa uhalisi
kile alichokuwa akikisema na kumaanisha.
Ukweli ni kwamba hauwezi kuwa
tofauti zaidi ya vile unavyowaza, unavyosema na kuchukua hatua kila siku
juu ya kile ulichotaka kufanya, hata kama ni kidogo namna gani; tambua
huleta matokeo halisi haijalishi ni matokeo chanya au ni matokeo hasi.
Kama ukiamua kuwaza na kuona mambo chanya uyatakayo katika maisha
yako, tena kwa imani; basi utakuwa umejiweka katika mazingira mazuri ya
kuweza kukabiliana na changamoto ya kutokushindwa juu ya kule
unapoelekea katika maisha yako. Suala la kushindwa kutimiza mipango
kadhaa kwenye muda uliojiwekea linaweza kujitokeza kwa wakati fulani,
hasa kama mipango hiyo imekuwa na njia pana za utekelezaji na kuhitaji
rasilimali nyinginezo zaidi zilizokuwa ngumu kupatikana kwa wakati huo.
Lakini tambua kuwa ndoto ya mtu haibadiliki, mipango yako itabadilika
ila si ndoto yako.
Badilisha mwelekeo wa namna unavyoona ndani yako; badilisha maneno
unayotamka na sababu unazozitoa katika kufikia ndoto yako. Anza kuona
upekee na utofauti ulionao ndani yako ambao Mungu amekupa kwa ajili ya
kufikia ndoto na kusudi la kuwepo kwako hapa duniani. Haya ndio maneno
madogo yenye madhara makubwa ya kukufanya usifikie mafanikio ya ndoto
yako uliyonayo.
1: Siwezi.
Neno siwezi limekuwa kama ukuta wa kuwazuia watu wengi kushindwa
kuendelea katika maisha yao na kufikia hatua ya mafanikio makubwa katika
malengo na mipango yao ya kila siku waliyonayo. Wapo watu wenye mipango
mizuri waliyoipanga lakini kila unapojaribu kuwapa mawazo mazuri zaidi
ya kuwasaidia kuwasogeza katika kupiga hatua juu ya kule wanapotaka
kuelekea, watakuambia hawawezi kufanya kile unachowashauri kufanya.
Unakutana na kijana aliyemaliza chuo kikuu na amekaa nyumbani kwa kukosa
ajira, lakini unapojaribu kumshauri atafute namna ya kujishughulisha
hata kwa biashara ndogo ndogo ili kutokupoteza muda wake; kijana huyo
atakujibu siwezi kufanya biashara kwa sababu mimi sikusomea masuala ya
biashara, na anazidi kukuambia unajua biashara ni kipaji mkuu.
Hapo panakuwa ni vigumu kuendelea kutoa msaada kwa sababu unaona
kabisa mtu huyu tayari amekwisha kutanguliza mawazo na fikira za
kushindwa juu ya jambo unalomshauri kufanya. Jambo hili ndio
linalowasumbua watu wengi hata kushindwa kuona matokeo chanya na
mafanikio wanayoyahitaji juu ya maisha yao. Usitegemee kuona mafanikio
katika maisha yako kama tayari unaona kushindwa ndani yako. Jifunze
kujaribu kila kitu kinachofaa na chenye kuleta matokeo chanya katika
maisha yako; heri kujaribu kuliko kukaa.
2: Naogopa.
Kila unapoambiwa uende ukasome uongeze ujunzi mpya unasema naogopa
nitaacha vipi familia yangu; mara naogopa kukaa mbali na familia yangu
kama nikienda kusoma. Hatimaye wenzako ulionao ofisi moja wanazidi
kupanda cheo na kukupita, hii ni kwa sababu wewe umeshindwa kujiongeza
na kurudi darasani kwa ajili ya kuongeza ufahamu kwa kisingizio cha
kuogopa utaachaje familia nyuma yako.
Hofu ya kushindwa, hofu ya kufanya mambo makubwa, hofu ya kukataliwa
na kuona aibu, hofu ya kutangulia mbele kwa niaba ya wengine kama vile
kuwa kiongozi; hii ndio inayokufanya usifikie ndoto yako nzuri uliyonayo
ndani yako kwa muda mrefu tangu miaka na miaka. Jiulize miaka na miaka
unaona aibu kufanya jambo zuri ulilonalo ndani ya moyo wako kwa
kisingizio cha kuogopa watu au kuona aibu; Swali, Je, kwa namna hiyo
utafanikiwa au utakula lini matunda ya ndoto yako uliyonayo? Je, Utaacha
historia gani katika dunia kama unaogopa kuishi na kutimiza ndoto ya
maisha yako hapa duniani. Badilika na kuwa mwenye ujasiri na njaa ya
kufanikiwa.
3: Nitafanya kesho.
Napoleon Hill aliwahi kusema kuwa, “Don’t wait. The time will never
be just right.” (Usisubiri. Hakuna kamwe muda muafaka wa kufanya
unachotaka. Akimaanisha kuwa muda wa kufanya unachotaka ni sasa na si
kesho. Wapo watu wengi sana wamekuwa ni wazuri katika kupanga na
kuongelea mipango yao waliyonayo kila siku, lakini si watu wepesi wa
kuchukua hatua juu ya mipango hiyo waliyonayo. Watu hawa kila
unapowafuata na kuwauliza ni kwa nini hawachukui hatua juu ya jambo
husika, watakuambia wanasubiri mambo yao yakae sawa, kwa hiyo watafanya
kesho au badae au mwakani.
Walt Disney aliwahi kuandika maneno mazuri yanayosema, “The way to
get started is to quit talking and begin doing.” (Njia nzuri ya kuanza
kufanya au kutekeleza unachotaka ni kuacha kuongea zaidi bali kufanya au
kuchukua hatua). Kama bado una miaka mitano au kumi unasema utaoa
mwakani na umri wako wa kuoa umefika na hauna kisingizio kwa nini hujaoa
hadi leo, basi ujue una matatizo mahali unahitaji uyaweke sawa kabla
hayajawa makubwa zaidi. Badilika acha kusema nitafanya kesho, nitafanya
kesho. Anza kufanya leo tena anza sasa baada ya kumaliza kusoma mahali
hapa. Huwezi kuibadili kesho kama hutoweza kuibadili leo.
4: Sina kipaji chochote.
Kuna rafiki yangu niliwahi kuishi nae, yeye alikuwa ni kama mfia
maji; anasema hana kipaji chochote kile anachoweza kukitumia kama sehemu
ya kumtambulisha. Nikamuuliza haujui hata kuimba, akanijibu sijui kwani
hata sauti niliyonayo haifai ni mbaya. Nilishangaa baada ya kuendelea
kumuhoji kwenye maeneo mengine na kila nilipomuhoji katika maeneo hayo
alinijibu hana na hata hawezi. Sijui kwa upande wako labda nikuulize na
wewe swali hili; Je, una kipaji gani unachoweza kukitumia kukutambulisha
mjini au mahali popote pale uendako hapa duniani? Kama jibu lako ni
kama la huyo rafiki yangu, basi unayo kazi.
Mara nyingi tumeona kipaji ndio kinachomtoa mtu na kumpa heshima kila
mahali anapokuwa au mahali anapokwenda. Mimi kipaji changu ni uandishi,
kutoa ushauri na kufundisha, ambayo mara nyingi ni mambo yanayoendana.
Swali ninalokuacha nalo tena ni hili; Je, wewe una kipaji gani
unachokijua hadi sasa unacho? Kipaji pekee ndio chenye uwezo wa kukupa
fedha, heshima na kukufanya kuwa kivutio kwa wengi. Amua leo kugundua
kipaji chako na acha kusema hauna kipaji; hakuna mtu aliyezaliwa duniani
iwe usiku au mchana ambaye Mungu hakumpa kipaji au kitu chochote kile
cha kufanya.
5: Umri wangu bado mdogo.
Wapo wanaosema umri wao ni mdogo na wapo wanaosema pia hawawezi
kufanya tena jambo fulani kwa sababu umri wao umekwenda yaani miaka yao
ya kufanya jambo husika imepita. Yote kwa yote sijui wewe upo upande
gani. Ila nataka kusema zaidi na wewe unayesema umri wako bado ni mdogo
na hauwezi kufanya jambo fulani kama vile, kuanza biashara au kujiajiri,
kuwa kiongozi wa nganzi fulani nchini, kushauri watu, nakadhalika. Huo
ni uongo ambao kamwe haustahili kuukubali kabisa ndani ya moyo na akili
yako; nataka nikumbie kama unauwezo wa kusoma makala hii au kuandika
hata herufi moja; basi tambua wewe unafaa kufanya kile unachotaka
(nielewe vizuri hapa kile unachotaka) kufanya maishani mwako. Sio lazima
ukitimize sasa bali unaweza kuanza kutengeneza mazingira ya kukifatilia
sasa na kukijengea misingi mizuri kuanzia sasa.
6: Elimu yangu ndogo au hainitoshi.
Kama elimu yako ni ndogo kwa nini usiweke malengo na mipango leo hii
ya kurudi kusoma tena na uchukue hatua ya haraka ya kufanya hivyo?
Usitoe nafasi ya jambo lolote linalowezekana kutimiza mbele yako kuwa
kisingizio cha kukuzuia kufikia ndoto yako uliyonayo moyoni. Kama una
nafasi ya kusoma hakikisha unasoma ili kuepuka kisingizio cha elimu
kuchukua nafasi ya kufikia ndoto na maono yako. Amua kuweka uamuzi upya
wa kurudi darasani; amua kuongeza elimu na ujuzi wako hata kwa kusoma
kozi fupi za nje ili uendelee kusoma huku ukifanya mambo yako mengine
uliyonayo. Badilika na zaidi amua kukimbia visingizio kama hivi visivyo
na tija, kama utakuwa fedha tafuta mazingira ya kuongeza ujuzi na
maarifa.
Hata kwako wewe ambae unasema hauna elimu, usitumie kigezo cha
kutokuwa na elimu kutokuishi kwa kutimiza ndoto yako uliyonayo. Ukisema
hivyo basi dunia ya sasa itakushangaa maana asilimia themanini na tano
ya matajiri wengi duniani elimu yao ni ya kawaida sana, na wengine kwa
kushangaza zaidi ulimwengu hata kwa kuwa na mafanikio makubwa pamoja na
elimu zao za darasa la saba na wamefanikiwa sana. Inawezekana kuifikia
ndoto yako kama utamua kutoka ndani ya moyo wako na kujiwekea malengo
timilifu utakayotembea nayo, ili kukupa hatua ya kufika mbali zaidi kule
unakotaka. Hakuna uchawi bali ni uamuzi wako; kubali na acha
visingizio.
7: Hao wameshaandikiwa kuwa matajiri tangu wamezaliwa. Mimi hataa sio wa upande huo.
Maneno yako ndio yanaonyesha wapi unapoelekea, na vitendo vyako
vinaleta uhalisi wa kile ulichokipanga. Hivyo basi, kumbe kwa maneno ya
kinywa cha mtu unaweza kumtambua mtu atakuwa wapi kwa miaka mitano hapo
badae, na kwa uamuzi wake wa kuchukua hatua ya utekelezaji utaona kwa
uhalisi kile alichokuwa akikisema na kumaanisha. Kama tayari umekuwa ni
mtu wa kukiri kuwa mafanikio ni ya baadhi ya watu fulani hapa duniani,
unategemea vipi kuona mafanikio hayo yakitokea katika maisha yako!
Usitegemee kupika nyama ya mbuzi wakati wa kula mezani ukategemea kuona
nyama ya kuku. Huo utakuwa ni muujiza mkubwa ambao haukuwahi kutokea
ulimwenguni kote.
Mara nyingi masikini huwa wanachukua nafasi ya kulalamikia watu
wanaofanikiwa na kuwaona kama si wenzao wanaoweza kuwa pamoja nao au
kupata msaada wowote kutoka kwao. Wakati unapoona mafanikio ni ya watu
fulani tu, ndio unapozidi kupunguza upeo wa akili yako katika kufikiri
na kuchukua hatua juu ya maisha yako. Jifunze kwa waliokutangulia na
acha kuwaona watu waliokutangulia kama sehemu ya watu fulani wa pekee
duniani. Amini nawe unaweza na amini daima unaweza kuliko mtu mwingine
yoyote yule.
Sababu na maneno mengine ni kama vile; sina hela ya kutosha nasubiri
nipate; sina muda wa kutosha nikipata muda nitafanya. Nakumbia kwa njia
yoyote ya sababu hizo na nyinginezo za maneno kama hayo, huwezi kuona
hatua yoyote utakayoipiga kwa ajili ya maisha yako na kufanikisha ndoto
yako uliyonayo. Kimbia visingizio na amini unaweza kuanzia sasa. Ushindi
ni kwa ajili yako; una nguvu; una uwezo mkubwa ndani yako; una muda;
una watu wa kukusaidia; kwa nini usitumie vitu vyote hivyo kama sehemu
ya kukusaidia kufanikiwa na kufikia ndoto yako. Amua leo hii na jiamini
kutoka katika moyo wako hakika utafika mahali unapotaka kufika.
Post a Comment