Nimesikitika sana kusikia Katibu Mkuu wa CECAFA anatafuta sehemu ya kufanyia mashindano haya (nchi mwenyeji), kila nchi inakwepa sababu gharama za kuendesha ni kubwa. Kama Ndondo Cup inakuwa na mvuto iweje Kagame ikose mvuto?, kweli viongozi wetu hawawezi kubadili mfumo wa uendesheshaji na mashindano yakarejesha mvuto wake?
Kagame Cup ingeendeshwa kwa mfumo wa ligi hakika ingekuwa na mvuto sana timu zingeaza kwa mtoano, baadaye makundi mfano kutoka timu 32 mpaka timu 8. Nasikitika mashindano makubwa kama hayo yanakosa wadhamini. Wakati Ndondo Cup ina Dr Mwaka, gazeti la Mwanaspoti n.k Kagame Cup inakosaje wadhamini? Mimi nafikiri ni wakati wa Bwana Nicholas Musonye kupumzika awapishe wengine waongoze ambao wataleta ubunifu kidogo (mawazo mapya).
Naamini mashindano haya yakiendeshwa kwa mfumo wa ligi wadhamini watapatikana. Kwa huu mfumo mbovu wa kucheza ndani ya wiki 1 au 2 ni ngumu sababu watu wanataka kutangaza biashara kwa muda mrefu. Siamini kama kuna mtu atadhamini tofauti na Rais Kagame sababu unakuta kwa siku kituo A zinacheza timu 4, B 4 na C 4 hayo kweli ni mashindano au bonanza? Hata bonanza linanafuu kidogo.
Mashabiki wa kuingia kila siku kuanzia saa 7 mpaka saa 12 wanatoka wapi?, je fedha/viingilio wanapata wapi vya kila siku? Mahitaji yao ya kila siku (nyumbani) wanapata wapi au hawana kazi za kufanya lakini viingilio vya kila siku wanapata? Ni maswali rahisi sana ya kujiuliza. Naamini mashindano haya yakiendeshwa kwa mfumo wa ligi Azam, Dangote, Vodacom nk hamtawakosa, wote hawa wanataka kutangaza biashara zao kwa muda mrefu.
Inashangaza sana Ndondo Cup inachezwa kwa zaidi ya miezi 4 lakini Kagame ya wachezaji ambao ni professionals inachezwa ndani ya wiki moja. Hapa tatizo ni mfumo mbovu wa uendeshaji usioendana na hali halisi, kinachohitajika ni ubunifu. Mashindano haya yakiendeshwa kwa mfumo wa ligi na ukateuliwa uwanja wa kufanyia fainali kama wanavyofanya ligi ya mabingwa Ulaya lazima kutakuwa na mvuto. Nakupongeza bwana Shaffi Dauda kwa ubunifu uliouonesha kwenye Ndondo mashindano yamekuwa na mvuto/mwitikio mkubwa sana mpaka tunaona viongozi wa serikali wakifika mara kwa mara.
Kagame Cup ikiendeshwa kwa mfumo wa ligi kuanzia mwezi wa 9 mpaka 12 miezi 4 inatosha kuendesha kabla ya mashindano ya CUF (CECAFA) acheni kutuharibia mashindano, hata UMITASHUMITA unakuwa na mvuto kuliko Kagame Cup sababu wanaanzia ngazi ya shule mpaka taifa.
Faida za mashindano yakiendeshwa kwa mfumo wa ligi
Wadhamini wataongezeka.
Mashabiki watakuwa na hamasa ya kuziona timu.
Gharama za uendeshaji zitakuwa chini sana.
Timu zitapata changamoto na mazingira mapya.
Mapato yataongezekana kutokana na mashabiki wa nchi mbalimbali kujitokeza.
Mashindano yatakuwa na mvuto wa hali ya juu sana.
Club zitapata wadhamini kwa ajili ya kutangaza biashara zao.
Wachezaji watapata uzoefu hata ikifika mashindano ya CUF wanakuwa na uzoefu wa kutosha.
Itakuwa ni kipimo kizuri kwa timu zetu.
Wachezaji watajitangaza n.k
Hitimisho
Viongozi wakubali kubadilika na wasikae muda mrefu madarakani maana wanakosa ubunifu badala yake wanaishi kwa mazoea, bwana Nicholas Musonye nimeanza kumsikia nikiwa sekondari mpaka leo nimekuwa babu hawezi kuwa na ubunifu tena, awapishe wengine ambao wataleta changamoto mpya au akubali kubadilika.

Post a Comment