0


Kama kuna mapinduzi ambayo kizazi hiki kinayashuhudia kwa macho basi ni mapinduzi ya kiteknolojia hasa kwenye kompyuta na mtandao wa intaneti. Mapinduzi mengi yaliyotokea huko nyuma hatukuwepo, tumekuwa tunayasikia tu kama mapinduzi ya viwanda.

Uzuri wa kuwa hai wakati wa mapinduzi ni kwamba unakuwa na nafasi kubwa ya kunufaika na mapinduzi hayo kuliko wale wanaokuja baadaye au waliochelewa kuyatumia mapinduzi hayo.

Kwa mfano watu wengi ambao wanashikilia rekodi ya kuwa matajiri sana duniani walitokana na mapinduzi ya viwanda yaliyotokea karne ya 19 ulaya na marekani.

Watu kama John Rockefeller walitumia vizuri mapinduzi ya viwanda kujijengea utajiri mkubwa.

Tukija kwenye zama zetu hizi za mapinduzi ya kiteknolojia, tunaona jinsi ambavyo mtandao wa intaneti umezalisha mabilionea wakubwa duniani.

Watu kama Mark Zuckerberg, mmiliki wa mtandao wa Facebook ni bilionea aliyezalishwa na mapinduzi haya ya kiteknolojia.

Wapo wengi ambao wananufaika sana na mapinduzi haya, swali ni je wewe unanufaikaje na mapinduzi haya? Hili ni swali muhimu tunalopaswa kujiuliza kila siku.

Mtandao wa intaneti umekuja na faida nyingi sana kwetu, kuanzia kuboresha kazi zetu, biashara zetu na hata maisha yetu kwa ujumla. Sasa hivi ni rahisi kutangaza biashara na hata kuwafikia wateja popote walipo duniani. Ni rahisi kuwasiliana na ndugu jamaa na marafiki popote pale walipo.

Lakini kila chenye faida hakikosi hasara, na mtandao wa intaneti umekuwa na hasara nyingi ambazo zimewazuia watu kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yao. Mtandao wa intaneti umekuwa na ulevi mkubwa hasa kwa watumiaji ambao unawafanya washindwe kuweka muda kwenye yale mambo ya muhimu kwao.

 Leo kupitia makala hii ya ushauri wa changamoto tutaona jinsi ya kuondokana na ulevi huu ili kuweza kutumia muda wetu vizuri na kufikia malengo yetu.

Kabla hatujaangalia kwa undani hatua za kuchukua, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusiana na changamoto hii.

Jambo la kwanza; kuwa na utaratibu maalumu wa kutembelea mitandao hii. 
Moja ya kitu kinachofanya matumizi ya mitandao kuwa changamoto ni ukaribu wake na urahisi wa kuitumia. Kwa kuwa mitandao hii ipo kwenye mikono yetu, nikimaanisha simu zetu za mkononi, ni rahisi sana kuingia hasa pale unapopata hata dakika moja.

Urahisi huu unafanya tukiwa na upweke kidogo tu tufungue mitandao. Baadaye tunaingiwa na hofu kamba tusipofungua muda mrefu basi tunapitwa, na hivyo tunajikuta kila baada ya dakika chache tunachungulia tena tuone kipi kipya.

Utafiti uliowahi kufanywa, kuhusiana na simu hizi za kiganjani, unaonesha watu wanazishika simu zao mara nyingi mno, na mara zote ni kwenye mitandao ya kijamii.

Ili kuondokana na ulevi huu, jiwekee utaratibu wa kuingia kwenye mitandao hii ya kijamii kwa muda fulani wa siku. usikubali kila dakika uwe ‘online’, jitengee muda maalumu kila siku au kila baada ya masaa fulani ndiyo uingie kwenye mitandao hii. Muda mwingine uweke kwa ajili ya kazi na zima kabisa data kwenye simu yako.

Unapokuwa kwenye kazi ambayo inahitaji umakini, usikatishe ili kuingia kwenye mitandao, kwani unaporudi kwenye kazi yako unapoteza muda mwingi zaidi.

Jambo la pili; ondoa taarifa za mitandao ya kijamii unazopata kupitia simu yako.
Kwenye simu zetu kuna kitu kinaitwa ‘notification’ hii ni ile taarifa ambayo simu yako inakupa kwamba kuna mtu kakutumia ujumbe, au kapenda picha yako kwenye mtandao.

Taarifa hizi zina nguvu ya kukusukuma uchukue hatua haraka kuona ni ujumbe gani umetumiwa au nani kasema nini kuhusu ulichoweka kwenye mitandao.

Ili kuondokana na hili, futa kabisa kupotea taarifa hizi za kila kinachoendelea kwenye mitandao. Kwa njia hii hutasukumwa kufungua badala yake utafungua pale muda wako uliojipangia unapokuwa umefika.

Na kama unaona huwezi kuondoa notification, ondoa kabisa zile application ambazo ni za mitandao ya kijamii, na badala yake uwe unaingia moja kwa moja kupitia mtandao. Siyo lazima uwe na app zote za kufungua kila aina ya mtandao, kwa sababu kwa kuwa nazo utajikuta umetengeneza utaratibu wa kuzunguka kwenye mitandao hii.

 Kwa mfano unaanza na facebook, unaangalia kisha unaenda instagram, ukimaliza unaenda snapchat, unatoka hapo unaingia wasap, kisha telegram, ukifika huko ni muda unarudi kuangalia tena kama kuna jipya facebook, kisha instagram, na unajikuta unarudia mzunguko mzima hata mara tatu. Ukiondoa zile app ambazo siyo muhimu sana utapunguza kutembelea ile mitandao ambayo siyo muhimu kwako.

Jambo la tatu; nufaika na mitandao hii. 
Kama umeshafanya njia hizo mbili lakini bado huwezi kujizuia kutembelea mitandao hii kila mara, basi angalia ni kwa namna gani unaweza kunufaika na itandao hii. Yaani angalia unawezaje kuitumia kujiingizia kipato.

Na habari njema sana kwako ni kwamba kila mtu, narudia tena KILA MTU anaweza kutengeneza kipato kupitia mtandao wa intaneti.

Kwa kuanza, angalia ni vitu gani unapenda sana kutembelea kwenye mitandao hii, ni vitu gani unapenda kufuatilia zaidi. Ukishajua vitu hivyo angalia ni kwa namna gani unaweza kuwasaidia wengine wanaohitaji taarifa zinazohusiana na vile unavyopenda kufuatilia. Na hapo unaweza kuanzisha ukurasa maalumu kwa ajili ya mambo hayo na hata kuwa na blog au tovuti.

Pia unaweza kutumia mitandao hii kuboresha kazi unayofanya au biashara yako. unaweza kutumia mitandao hii kupata wateja wa kile unachofanya au kutoa taarifa kwa wale wanaohusika na unachofanya. Pia unaweza kutumia mitandao hii kufanya tafiti zinazohusu kazi au biashara yako. zipo njia nyingi za kunufaika ni wewe kuchagua kipi kinakufaa.

Post a Comment

 
Top