0
Wakati kukiwa na ulinzi mkali mjini Dodoma kuelekea Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) limehamishia mkutano wake wa kamati ya utendaji jijini Dar es Salaam.

Jana, sekretareti ya CCM ilianza maandalizi kusafisha njia kwa ajili ya kikao cha Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na baadaye Mkutano Mkuu uliopangwa kufanyika Jumamosi.

Awali, Bavicha ilikuwa imehamasisha vijana wa chama hicho kuja kwa wingi mjini hapa kwa ajili ya “kutekeleza agizo la Rais John Magufuli kuzuia mikutano ya kisiasa”, lakini Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alifuta mpango huo akisema: “Waache wafu wawazike wafu wao”.

Pamoja na Mbowe kuzuia, Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi alisema wiki iliyopita kuwa wameandaa mkutano wa Kamati ya Utendaji wa Baraza hilo leo mjini Dodoma na ungefunguliwa na Mbowe.

Huku ulinzi ukizidi kuimarishwa, jana kulikuwa na uamuzi tofauti.

Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Dodoma, Malambaya Manyanya jana alisema wameamua kuuhamishia mkutano huo Dar es Salaam baada ya kuona mzozo umekuwa mkali.

"Tumeona mzozo ni mkali sana. Tumeona imeshakuwa shida, tukaona ngoja tukafanyie Dar,” alisema Manyanya.

Alisema wajumbe waliokuwa waingie Dodoma jana, wameambiwa wote waelekee Dar es Salaam  kwenye jengo la makao makuu

Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka yeye anasema kutakuwa ulinzi mkali na hakuna atakayeweza kujaribu kuvuruga mkutano huo ambao utashuhudia Rais John Magufuli akichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho.

Ole Sendeka alisema kwenye ukumbi mpya wa CCM ambako ndiko mkutano huo utakafanyika, kutakuwa na kamera maalumu zitakazofungwa ndani na nje ya ukumbi ili kuwezesha kuona kila kitu kinachoendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa mkoa, alisema ameona kwenye mitandao ya kijamii kwamba baadhi ya vyama vinatoa vitisho na kuwataka wananchi wavipuuze.

 “Na kama kuna mtu anadhani kuwa anaweza kukwamisha mkutano mkuu wa CCM, nimwambie Dodoma si salama kwake. Afikirie mahali pengine, lakini si Dodoma,” alisema.

“Nitumie fursa hii kuwaomba wananchi pale wanapoona mtu wasiyemwelewa au dalili waripoti haraka kwenye vyombo vya habari na dola au kwa viongozi popote pale ambapo wanaweza kushirikiana kuliondoa hilo tatizo. Lakini kwa ujumla hali iko shwari mpaka sasa,” alisema Rugimbana.

 Wakati Rugimbana akisema hayo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Mayalla Towo amesema wameweka miundombinu ya kuweza kuwabaini wahalifu, lakini hawezi kuitaja.

Post a Comment

 
Top